1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joto la 2023 halikuwahi kushuhudia miaka 100,000 iliyopita

10 Januari 2024

Mamlaka ya kufuatilia mabadiliko ya tabianchi barani Ulaya inasema 2023 ulikuwa ndio mwaka wenye joto kali zaidi kuwahi kurikodiwa duniani, ambapo lilikikaribia kuvuuka ukomo wa nyuzi 1.5 kwa kipimo cha Celsius.

Moto kwenye msitu wa Australia mwezi Novemba 2023.
Moto kwenye msitu wa Australia mwezi Novemba 2023.Picha: DFES /AP/picture alliance

Taarifa iliyotolewa siku ya Jumanne (Januari 9) na Taasisi ya Copernicus Climate Change Service ilisema kwamba mabadiliko ya tabianchi yalizidisha kiwango cha joto, ukame na moto kwenye misitu kote duniani na kukipelekea kiwango cha joto la ulimwengu kufikia hadi nyuzi 1.48 kwa kipimo cha Celcius.

"Huu pia ulikuwa mwaka wa kwanza ambapo siku zote zilikuwa na ongezeko la nyuzi moja ya joto kuliko kilivyokuwa kipindi cha kabla ya mapinduzi ya viwanda duniani. Hali ya joto kwenye mwaka wa 2023 ilipindukiwa kipindi chochote kile ndani ya miaka 100,000 iliyopita." Alisema Samantha Burgess, naibu mkuu wa taasisi hiyo, mjini Paris, Ufaransa.

Soma zaidi: UN: Kuelekea COP28 ulimwengu wapambana na mafuta ya visukuku

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema mwaka jana ulikuwa ni kipimo tu cha janga kubwa zaidi ambalo dunia itakumbana nalo, endapo hatua hazikuchukuliwa sasa. 

Kwa mujibu wa wanasayansi, takribani nusu nzima ya mwaka 2023 ilishuhudia joto likiwa juu ya nyuzi 1.5, kiwango ambacho kama kikipitwa, basi mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha majanga makubwa zaidi kuliko ambayo yameshashuhudiwa hadi sasa.

Mwaka wa joto na moto

Mwaka 2023 ulishuhudia moto mkubwa ukiwaka kwenye misitu ya Canada, ukame mkubwa kabisa kwenye Pembe ya Afrika na Mashariki ya Kati, joto kali kwenye majira ya kiangazi barani Ulaya, Marekani na China, huku Australia na Amerika Kusini zikipata majira ya kipupwe yenye joto.

Mkaazi wa Rio de Janeiro akijitia maji mtaani kutokana na joto kali mwezi Novemba 2023.Picha: TERCIO TEIXEIRA/AFP/Getty Images

Mwaka huo pia ulishuhudia mwanzo wa hali mbaya ya hewa ya El Nino, ambayo inayafanya maji kwenye eneo la kusini mwa Bahari ya Pasifiki kupata joto na matokeo yake kuchochea hali ya joto kali kwengineko ulimwenguni.

Soma zaidi: Umoja wa Mataifa wahofia mizozo na majanga kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi ulimwenguni

Hali hiyo inatazamiwa kufikia ukomo wake mwaka huu wa 2024, ambapo inakisiwa kuwapo kwa miezi minane mfululizo, kutoka Juni hadi Disemba.

Profesa wa Mabadiliko ya Tabianchi katika Chuo Kikuu cha Reading, Ed Hawkins, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba "matukio kama hayo yataendelea kujiri hadi pale dunia itakapoachana na matumizi ya nishati za visukuku na kufikia lengo la kuondosha hewa chafu katika tabakahewa."

Soma zaidi: Mafuriko Kongo yaendelea kuathiri wakaazi

Ugunduzi huo wa taasisi ya Corpenicus umetangazwa ikiwa ni mwezi mmoja tu baada ya makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Dubai mwaka jana, COP28, ambayo yalitaka dunia kuachana na nishati za visukuku hatua kwa hatua.

Hata hivyo, hata kama kiwango hicho kitavuuka ukomo wa 1.5 katika mwaka huu wa 2024, taarifa ya Taasisi ya Copernicus ilisema hilo halitamaanisha kwamba dunia imeshindwa kufikia malengo ya Makubaliano ya Paris ya kudhibiti joto ulimwenguni.

Vyanzo: AFP,AP