Joto la dunia kuongezeka hadi nyuzi joto 1.5
8 Oktoba 2018Jopo la kiserikali kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC, limetoa ripoti maalum leo ikionya kuhusu madhara ya kukosa kufikia lengo hilo, miezi miwili kabla ya mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi. Tathmini hiyo inaonesha kuwa waangalizi wameona athari za mabadiliko ya nyuzi 1, na kutaja mabadiliko hayo kuwa hali ya hewa iliyokithiri, kupanda kwa usawa wa bahari, na kupotea kwa barafu katika eneo la Arctic.
Chini ya ya lengo hilo, wataalamu wanasema usawa wa bahari hautapanda kwa zaidi ya sentimita kumi. Vile vile itapunguza uwezekano wa bahari ya eneo la Arctic lisilo na barafu msimu wa joto, na miamba ya matumbawe kupungua kwa kati ya asilimi 70 hadi 90, kinyume na kupotea kabisa iwapo joto litaongezeka kwa nyuzi 2.
Ripoti hiyo aidha inaonesha kuwa sera ya mabadiliko ni muhimu katika ardhi, kawi, viwanda, majengo, usafiri na miji, na kaboni dioksidi inayotolewa na binadamu inafaa kushuka kwa asilimia 45 kutoka viwango vya mwaka 2010 ifikapo mwaka 2030 ili kuafikia lengo la chini.
Mwenyekiti wa IPCC Hoesung Lee, amesema mabadiliko ya hali ya hewa yanawaathiri watu, mazingira na maisha yao kote duniani. ´´Kupunguza joto hadi nyuzi 1.5 inawezekana lakini itahitaji mapito yasiykuwa ya kawaida katika vipengele vyote vya jamii. Kuna manufaa ya wazi kwa kuweka kiwango cha joto hadi nyuzi 1.5 ikilinganishwa na nyuzi mbili au zaidi. Kila kiwango ha joto kina umuhimu.´´
Ripoti hiyo inasema viwango vya Kaboni Dioksidi vinafaakufikia kile alihokiita ´´net zero´´ ifikapo mwaka 2050 . Hii ina maana gesi itakayotolewa inafaa kuondolewa hewani, kwa kutumia technolojia inayojulikana kama kukamatwa kwa kaboni ambayobado ni changa.
Makubaliano ya Paris ya mwaka 2015 yaliangazia juhudi za kuhakikisha kuongezeka kwa joto kunasalia chini ya nyuzi mbili na kuzingatia mbinu za kudhibiti ongezeko la joto hata zaidi hadi nyuzi 1.5. Marekani ambayo ni mtoaji mkuu wa Kaboni Dioksidi ilijitoa kwenye mkataba huo wa Paris mwaka uliopita, hivyo kuzua wasiwasi kuhusu ufanisi wake.
Watafiti wengi wanasema iwapo hakuna hatua yoyote itakayochukuliwa kupunguza utoaji wa gesi, dunia itaendelea kupitia njia ya joto la dunia ambayo inaweza kufika nyuzi 3 au 4. Mawaziri wa mazingira wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukamilisha majadiliano kuhusu misimamo yao katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa ya Desemba jijini Katowice, Poland, kuhusu utekelezaji wa mkataba wa mwaka 2015.
Kamishna wa Masuala ya Hali ya Hewa wa Umoja wa Ulaya Miguel Canete alitaka kuongeza lengo la mwaka 2030 hadi asilimi 45 ikilinganishwa na mwaka 1990, lakini hatua hiyo imepingwa na Ujerumani na mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/DPAE
Mhariri: Iddi Ssessanga