Jubaland kuungana na serikali ya Somalia
29 Agosti 2013Habari hiyo inapokewa vyema na mataifa yanayoisaidia Somalia, ambayo yamekuwa katika jitihada kuifanya serikali yake kufikisha mkono wake katika maeneo ya mbali na Mogadishu, vilevile kukabiliana na wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab, lenye mfungamano na Al-Qaeda.
Jubaland eneo ambalo lipo kusini mwa Somalia na kupakana na Kenya, lilikuwa miongoni mwa maeneo yaliojitenga katika taifa hilo tete la Pembe ya Afrika. Vilevile kuna eneo la Puntland kwa upande wa kaskazini/mashariki ambalo linataka mamlaka yake ndani ya serikali ya shirikisho, wakati Somaliland ilijitangazia uhuru wake tangu 1991.
Kilichomo katika makubaliano
Makubaliano haya ya sasa yamesainiwa baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takribani wiki moja kati ya waziri wa nchi wa Somalia, Farah Sheikh Abdulkadri, na kiongozi wa Jubaland aliyejiteuwa mwenyewe Ahmed Madobe.
Serikali ya shirikisho ya Somalia na ujumbe wa Jubaland wamekubaliana kuunda utawala wa mpito katika eneo hilo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo Madobe ataendelea kuwa kiongozi wa eneo hilo kwa kipindi cha miaka miwili lakini hajakubali kuacha udhibiti wa bandari na uwanja wa ndege katika eneo la Kismayo.
Ahadi za kiongozi Madobe
Madobe vilevile ameahidi kuunganisha vyombo vya usalama wakiwemo wanamgambo wake na jeshi la taifa, ambalo linaungwa mkono na wanajeshi 17,700 wa Umoja wa Afrika waliyopo nchini humo. Kiongozi huyo ambae alijitangza kuwa ndiye rais wa Jubaland mwezi Mei ameahidi kutimiza masharti ya makubaliano hayo.
Baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo Madobe alisisitiza kwa kusema " Nataka kuwahakikishia, sijasimama hapa kusema mambo ambayo baadae hatuyatekelezi. Natumanini jambo hili litatekelezwa kwa vitendo na litakuwa jema kwa Somalia yote". Alisema kiongozi hiyo.
Upande wa serikali nao ulisema wamekubalina si katika pande mbili zenye kuijenga Somalia, bali katika pande moja yenye kujenga serikali ya shirikisho ya taifa hilo.
Hata hivyo baadhi ya vifungu zaidi kuhusu makubaliano hayo vitakamilishwa katika mazungumzo mengine yanayotarajiwa kufanyika mjini Mogadishu ambayo hata hivyo tarehe yake bado haijapangwa.
Umoja wa Mataifa watoa onyo
Mwakilishia maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ameyakaribisha makubliano hayo huko na kutoa tahadhari zake.
Akizungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP, Nick Kay amesema wanapaswa kuwa na matumaini makubwa, lakini pia kuweka tahadhari muda wote kwa kuwa hali ya Somalia imekuwa ngumu kutoka na historia yake kwa hivyo watayafuatilia kwa kina makubaliano hayo.
Serikali ya mpya ya Somalia imekuwa ya kwanza kutambuliwa kimataifa tangu kuanguka ile ya mwaka 1991. Lakini imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa katika miezi ya hivi karibuni yakiwemo mashambulizi ya Al-Shabaab, tuhuma za ubakaji kwa jeshi lake na Umoja wa Afrika na kuondoka kwa wafanyakazi mashirika ya kutoa misaada ya kimataifa kutokana na wimbi la vitendo vya utekaji nyara na ubakaji.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Josephat Charo