1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi mpya zaanzishwa ili kusitisha mapigano Gaza

22 Februari 2024

Juhudi mpya za kutaka kusitishwa mapigano kwenye Ukanda wa Gaza zimeanzishwa katika wakati makabiliano kati ya vikosi vya Israel na kundi la Hamas bado yamechachamaa kwenye eneo hilo.

Ukanda wa Gaza | Moshi ukifuka kutoka kitongoji cha Khan Yunis
Moshi ukifuka kutoka kitongoji cha Khan Younis katika Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi yanayoendelea ya Israel eneo hilo: 22.02.2024Picha: SAID KHATIB/AFP/Getty Images

Wizara ya afya huko Gaza inayodhibitiwa na Hamas imesema watu 94 wameuawa huko Gaza katika muda wa saa 24 zilizopita, na hivyo idadi jumla ya vifo ikifikia watu 29,410 tangu kuanza kwa  mzozo huu kati ya Israel na Hamas  Oktoba 7, 2023.

Mapema leo asubuhi watu watatu wenye silaha walifyatua risasi kwenye barabara iliyo karibu na kituo cha ukaguzi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Israel, na kuua Muisraeli mmoja na kuwajeruhi wengine wanane. Washambuliaji wawili waliuawa na mmoja alikamatwa na sasa anashikiliwa na polisi.

Soma pia: Shirika la mpango wa chakula duniani WFP lasitisha ugawaji chakula kaskazini mwa Gaza

Mjumbe wa Baraza la Vita la Israel Benny Gantz, amesema usiku wa jana kwamba kumekuwepo majaribio mapya yanayolenga kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas, ambayo amesema yanaweza kusitisha vita huko Gaza. Lakini Gantz amesisitiza kuwa hilo litawezekana ikiwa tu Hamas itakubali kuwaachilia mateka wa Israel waliosalia kwenye Ukanda wa Gaza.

Raia wa Palestina wakishuhudia uharibifu mkubwa baada ya mashambulizi ya Israel katika msikiti wa Af Farouf karibu na Rafah kusini mwa GazaPicha: Ahmed Zaqout/Anadolu/picture alliance

Mnamo majuzi, Israel ilitishia kuwa itaanzisha mashambulizi ya ardhini katika mji wa kusini mwa Gaza na wenye watu wengi wa  Rafah  katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani. Stephane Dujarric, Msemaji wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameielezea hali mbaya inayoendelea huko Gaza:

" Washirika wetu wa kibinadamu wanaoshughulikia masuala ya maji, usafi wa mazingira na afya huko Gaza walionya jana kwamba hatua za haraka zinahitajika ili kukabiliana na janga la kiafya linalotokea katika Ukanda wa Gaza. Watu wengi hawajapata maji safi, na moja tu ya mabomba matatu kutoka Israel ndio bado yanafanya kazi, tena ikiwa chini ya nusu ya uwezo wake wa kawaida. Takriban asilimia 83 ya visima havitumiki tena huko Gaza, huku mifumo ya maji taka ikiwa yote haifanyi kazi."

Miito ya usitishwaji mapigano huko Gaza yatolewa

Mkutano wa Mawaziri wa mambo ya nje wa G20 unaoendelea huko BrazilPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Wakati wa mazungumzo katika mkutano wa G20 huko Brazil, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua jukumu kubwa la kushinikiza usitishaji haraka wa vita vya Gaza na pia kuwepo kwa suluhu ya mataifa mawili.

Soma pia: Vurugu bungeni Uingereza kwa maazimio ya Gaza

Wito kama huo umetolewa pia na Mratibu wa Shirika la Misaada ya Dharura la Umoja wa Mataifa Martin Griffiths ambaye amewataka mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 20 zilizoendelea na kustawi kiviwanda kuchukua hatua za kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza.

Jana, Bunge la Israel liliunga mkono kwa wingi pendekezo la Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu la kupinga uamuzi wa upande mmoja wa kutambuliwa kwa taifa la Palestina. Netanyahu amekuwa mara kadha akisisitiza kuwa Israel itaendeleza mashambulizi yake huko Gaza hadi watakapopata kile anachokiita "ushindi kamili".

(Vyanzo:afp,ap,rtr,dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW