1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za Amani ya Mashariki ya Kati Zashika Kasi

1 Aprili 2014

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amemaliza ziara ya masaa karibu 16 mashariki ya kati bila ya kukutana na kiongozi wa mamlaka ya utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry aaondoka tel AvivPicha: Reuters

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amekutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa mara ya pili hii leo baada ya kupita masaa 12-ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuyanusuru mazungumzo kati ya Israel na Palastina yasivunjike.

Jana John Kerry alisitisha ziara yake ya Ulaya na kwenda Jerusalem ambako alikutana kwa muda mrefu kwanza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na baadae na mkuu wa tume ya Palastina katika mazungumzo ya amani Saeb Erakat baada ya mazungumzo pamoja na Mahmoud Abbas kuakhirishwa jana usiku.

Baada ya duru ya pili ya mazungumzo leo asubuhi pamoja na Netanyahu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani ameondoka na kwenda Brussels kuhudhuria mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa jumuia ya kujihami ya NATO kuhusu Ukraine na Afghanistan.

Maafisa wa kipalastina wanasema hata hivyo waziri Kerry huenda akarejea katika eneo hilo kesho ili kukutana na kiongozi wa utawala wa ndani Mahmoud Abbas.

Kila upande unataka hakikisho

Jana wapalastina wameitaka Marekani iwape hakikisho la kuachiliwa huru kundi la tatu na la mwisho la wafungwa wa kipalastina waliokuwa waachiwe huru Marchi 29 iliyopita.Israel inapinga kuwaachia huru ikitaka ipatiwe hakikisho na wapalastina kwamba hawataondoka katika meza ya mazungumzo wafungwa hao wakiachiwa huru.

Wakuu wa tume za Israel na Palastina katika mazungumzo ya amani:Tzipi Livni (kushoto) na Saeb ErakatPicha: picture-alliance/dpa

Duru za kuaminika zinasema Marekani inafikiria uwezekano wa kumuachia huru jasusi Jonathan Pollard anaeshikiliwa Marekani ili kuyanusuru mazungumzo ya amani.

Jana usiku uongozi wa wapalastina ulikutana Ramallah,akihudhuria pia Mahmoud Abbas na kutishia kuendelea na juhudi za kujiunga na mashirika ya Umoja wa mataifa ikiwa hawatapatiwa hakikisho la kuachiwa huru wapalastina hao katika kipindi cha masaa 24 yanayokuja.Wamepinga pia fikra ya kurefushwa mazungumzo ya amani,baada ya Aprili 29 bila ya kwanza Israel kusitisha ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika ukingo wa magharibi wa mto Jordan na katika sehemu ya mashariki ya Jerusalem.Zaidi ya hayo wapalastina wanataka wafungwa elfu moja ziada wa kipalastina akiwemo Marwan Barghouti na Ahmad Saadat waachiwe huru.Israel lakini inasemekana inapendekeza kuwaachia huru wafungwa 420, kufungua njia ya mpakani kati ya Ukingo wa magharibi na Jordan na kuruhusu kuishi pamoja familia.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir:Reuters/DPA/AFP

Mhariri. Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW