Juhudi za kuepusha kitisho cha hujuma za Uturuki kaskazini mwa Irak
23 Oktoba 2007Juhudi za kidiplomasia zimeshika kasi mjini Baghdad hii leo,kuepukana na balaa la hujuma za kijeshi za Uturuki dhidi ya vituo vya waasi wa kikurd kaskazini mwa Irak.
Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan yuko ziarani mjini London kwa mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Uengereza Gordon Brown.Na waziri wake wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki,Ali Babacan akaelekea Baghdad kwa mazungumzo pamoja na waziri mkuu wa Irak Nouri El Maliki,rais Jalal Talabani na waziri mwenzake Hishyar Zebari.Katika mkutano pamoja na waandishi habari,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Irak alimhakikishia mgeni wake wa Uturuki,Irak “inawaunga mkono katika mapambano yao dhidi ya kitisho cha waasi wa kikurd.”
Ziara hizi ni katika juhudi za kutahadharisha dhidi ya kitisho kinachoweza kutokana na mashambulio ya waasi wa PKK dhidi ya Uturuki.
Jana usiku rais George W. Bush ,alizungumza kwa simu na kiongozi mwenzake wa Uturuki Abdallah Gul,na kumhakikishia serikali yake inazingatia uwezekano wa kushirikiana na Uturuki ili kukomesha mashambulio ya waasi wa kikurde .
Waziri mkuu Racep Tayyib Erdogan amefika hadi ya kuzungumzia juu ya opereshini ya pamoja ya kijeshi kati ya Uturuki na Marekani .
Wakati huo huo Marekani na Uengereza,kwa pamoja zimewatolea mwito viongozi wa serikali ya Irak wapitishe hatua za haraka kuzuwia mashambulio ya wanamgambo wa kikurd dhidi ya raia wa Uturuki.
Baada ya mazungumzo pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uengereza David Miliband, mjini Washington: waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani bibi Condoleezza Rice alisema:
“Marekani imedhamiria kushirikiana pamoja na washirika wake wote nchini Irak na nchini Uturuki ili kujaribu kukabiliana na hali tete ya ugaidi kutoka eneo la mbali la kaskazini mwa Irak.”
Kwa mujibu wa gazeti la Chicago Tribune lililowanukuu maafisa wa ngazi ya juu ,serikali ya Marekani inafikiria uwezekano wa kufanya mashambulio ya angani dhidi ya waasi wa PKK ili kuepusha balaa la kuingilia kati kijeshi Uturuki.
Mzozo huu unaishughulisha sana Marekani inayohofia pindi Uturuki ikiingilia kati kijeshi nchini Irak,vurugu litaenea hata katika yale ambayo zamani yalikua salama nchini Irak.
Jana usiku waasi wa PKK wamesema wako tayari kuweka chini silaha ikiwa jeshi la Uturuki litaachana na azma yake ya kulivamia eneo la kaskazini la Irak na kama Uturuki itaheshimu haki za kisiasa na kitamaduni za jamii ya wachache ya wakurd.
Kabla ya kuwasili Baghdad,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Ali Babacan alikua ziarani Kuweit alikosema nchi yake inatanguliza mbele mazungumzo kusaka ufumbuzi wa mzozo wa waasi wa wakurd.Matamshi hayo hayo ameyatoa hivi punde wakati wa mkutano na waandishi habari mjini Baghdad.