1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kufufua kilimo cha korosho Pwani ya Kenya

Josephat Charo
22 Oktoba 2018

Vijiji vya Rabai katika kaunti ya Kilifi vina utajiri mkubwa ambao ni ardhi yenye rutuba. Wakulima wana matumaini mapya baada ya serikali ya kaunti kuzindua mradi maalum wa kufufua kilimo cha korosho kuimarisha pato lao.

Kenia Nairobi Landwirtschaft
Picha: DW/T. Mwadzaya

Kijiji cha Mwawesa kilichoko eneo la Rabai kina utulivu mwingi kwani wakazi wake aghalabu ni wakulima. Baadhi wanapanda mboga, minazi, mahindi na mimea miengine. Kilimo cha korosho kilikuwa na pato kubwa kwa wakazi wa kaunti za Kilifi na Kwale miaka 20 iliyopita ila biashara ilisambaratika. Kwa mujibu wa gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Kingi dhamira ni kuzinyanyua hali za wakazi wa pwani kadhalika kuunda ajira kwa vijana. Boniface Nganga, ndiye mratibu wa mradi wa kufufua kilimo cha mikorosho katika wadi ya Mwawesa iliyoko eneo la Rabai la kaunti ya Kilifi.

Mradi huu wa miaka mitano unaungwa mkono na mashirika yasiyo ya kiserikali ukizingatia maelezo ya kitaalam, kilimo na biashara yenyewe ya kuuza korosho. Mashirika hayo ni pamoja na Emergency Trust Fund for Africa, Farm Africa na Ten Senses. Wakulima tayari wameshapokea miche ya kisasa na kuipanda zikiwa ni hatua za mwanzomwanzo za kufanishika mradi. Baadhi ya wakulima ambao wameshapokea miche kijijini Mwawesa walielezea mtazamo wao na pia hali halisi.

Kutoka kulia, Eunice Kadzo Ngumbao, Afisa wa Kilimo, Boniface Nganga, Mratibu wa wadi ya Mwawesa, kaunti ya Kilifi na mkulima wa Mwawese, Nyamvula RamadhanPicha: DW/T. Mwadzaya

Awali wakulima walikuwa na tashwishi na mpango wenyewe kwa kuzingatia kuwa biashara ilisambaratika zaidi ya miongo miwili iliyopita. Kwa mujibu wa wataalam aina hii mpya ya mbegu ya mikorosho inahitaji muda wa miaka 2 pekee kukomaa. Tsomnyazi Nganga ni mwanasayansi na mtaalam wa ukuaji wa mimea anayejihusisha na jitihada za kukifuafua kilimo cha mikorosho pwani ya Kenya.

Mikorosho kupandwa na mimea mingine

Kulingana na washauri wa kilimo, mikorosho inaweza kupandwa pamoja na mimea miengine kwenye shamba hilohilo moja. Hilo linamuwezesha mkulima kuvuna mara mbili kadhalika kulinda mazingira. Eunice Kadzo Ngumbao ni mshauri wa kilimo katika eneo la Rabai katika kaunti ya Kilifi na alielezea juu ya mambo yanayopaswa kufuatwa wakati wa kuipanda miche.

Mkulima wa Mwawesa akiwa na mbegu ya mkorosho ambao haukuota kwa sababu ulipandwa kwenye mfuko wa plastikiPicha: DW/T. Mwadzaya

Kwa upande wake serikali ya kaunti ya Kilifi inashirikiana na wadau wa kundi la Visegrad ambao wanafadhili mradi wenyewe kupitia washirika wa maendeleo. Kundi hilo linayajumisha mataifa ya Hungary, Jamhuri ya Czech, Poland na Slovakia. Hata hivyo wanaharakati wa masuala ya kijamii wanahoji kuwa ipo haja ya kuwashirikisha wanakijiji moja kwa moja. Hii ni kwa sababu hiyo ni moja ya njia za kuishinikiza serikali kulitambua zao la korosho kama moja ya mazao yanayoweza kuchangia katika pato la kitaifa. Masai Mawira ni mshauri wa kilimo na mwanaharakati wa masuala ya jamii katika eneo la pwani na anafafanua.

Juhudi zimeshika kasi

Kwa sasa harakati zinaendelea kuishinikiza serikali kufanikisha mapendekezo ya jopo kazi la Mumba lililotathmini hali iliyosababisha kampuni ya korosho ya Kenya kusambaratika katika miaka ya tisini. Mwaka 2009 serikali ya Kenya iliunda jopo kazi la washirika 5 kutathmini njia mujarab za kuifufua sekta ya korosho chini ya usimamizi wa John Safari Mumba aliyewahi kuwa mbunge wa Bahari na mkurugenzi mkuu wa kampuni ya korosho ya Kilifi iliyosambaratika. Baada ya kupokea ripoti ya jopo kazi hilo, serikali ilipiga marufuku mwaka huohuo uuzaji wa korosho ambazo hazijabanguliwa ili kumnusuru mkulima na mawakala walafi.

Mkorosho uliozeeka huko Gazi, kautni ya KwalePicha: DW/T. Mwadzaya

Juhudi za kuifufua sekta ya korosho zilianza tangu mwaka 2013 ila kwa sasa ndio utekelezaji umeanza rasmi. Matumaini ya wakulima ni kuwa waweze kulipwa moja kwa moja pasina vikwazo.Shirika la biashara ya kilimo Ten senses limekuwa likishirikiana na wakulima wa pwani kuuza bidhaa za njugu kama vile mtama, macadamia na sasa korosho. Frank Omondi, mkurugenzi mkuu wa Ten Senses Africa aliweka bayana mipango iliyopo.

Kwa sasa mikakati inaendelea kuunda kiwanda cha kutengeza bidhaa za korosho kwa madhumuni ya kuziongezea thamani jambo litakaloziongeza bei katika soko lolote lile.Hadi hapo msikilizaji, hatuna cha ziada,Tumeangazia juhudi za kufufua kilimo cha korosho katika eneo la pwani ya Kenya kwa manufaa ya wakazi wake.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Josephat Charo