1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kufungua njia za usafirishaji chakula zashika kasi

13 Julai 2022

Urusi,Ukraine,Uturuki na Umoja wa Mataifa kujadili njia ya safari za meli za vyakula zilizokwama katika bandari za Ukraine

Ukraine Transport von Getreide
Picha: Vadim Ghirda/AP Photo/picture alliance

Ujumbe wa maafisa wa kijeshi kutoka Urusi,Ukraine na Uturuki wanakutana hii leo na maafisa wa Umoja wa Mataifa mjini Istanbul Uturuki kwa mazungumzo  kuhusu uwezekano wa kupatikana makubaliano ya kufunguliwa tena njia salama  za kusafirisha nafaka kutoka bandari kuu ya bahari nyeusi.

Picha: Lyashonok Nina/Ukrinform/ABACA/picture alliance

Mkutano huo wa leo ni muhimu kufuatia hali ya ukosefu wa chakula ulimwenguni inayoshuhudiwa hivi sasa kufuatia vita nchini Ukraine. Wanadiplomasia wameeleza kwamba yaliyomo kwenye mpango unaojadiliwa yanajumuisha suala la meli za Ukraine zinazosindikiza meli za kubeba shehena za nafaka zinazoingia na kutoka  kupitia bandari ya Odesa, Urusi kukubali usitishaji mapigano wakati meli hizo zikisafiri kwenye eneo hilo na kwa upande mwingine Uturuki ikishirikiana na Umoja wa Mataifa zitafanya ukaguzi wa meli hizo ili kuiondolea wasiwasi Urusi kuhusu uingizwaji silaha kimagendo.

Uturuki imekuwa ikishirikiana na Umoja wa Mataifa kusimamia mpango huo baada ya uvamizi wa Urusi Februari 24 kusababisha bei ya nafaka, mafuta ya kupikia, mafuta ya petroli na mbolea kupanda dunia nzima. Waziri wa ulinzi wa Uturuki Hulusi Akar ndiye aliyetangaza jana juu ya kufanyika mkutano huu lakini pia hapo jana katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Gutterres aliwaambia waandishi wa habari kwamba wanafanya kazi kubwa sana lakini bado yapo matumaini na wataendelea kujaribu.

Picha: Ukrainian Armed Forces/REUTERS

Hata Ukraine nayo pia jana ilionesha kuwa na matumaini ya kuongeza usafirishaji wa nafaka licha ya kuweko vizuizi vya Urusi katika bandari zake za bahari nyeusi. Ukraine ilisema kwamba meli zake zilianza kusafiri kupitia njia muhimu ya mto Danube. Ukraine na Urusi ni wasafirishaji wakubwa duniani wa ngano na Urusi ikiwa pia msafirishaji mkubwa wa mbolea na kwa upande mwingine Ukraine ikiwa mzalishaji muhimu wa mafuta ya kupikia yanayotokana na mahindi na alizeti.

Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine pamoja na hatua ya kuweka vizuizi kwenye bahari nyeusi upande wa Ukraine ni mambo yaliyokwamisha shughuli za usafirishaji na kusababisha meli chungunzima kukwama na tani zaidi ya milioni 20 za nafaka zimekwama katika bandari ya Odesa. Na mavuno yanayokuja pia yanakabiliwa na mashaka katika wakati ambapo Ukraine hivi sasa inakabiliwa na uhaba wa maeneo ya kuhifadhi mazao kufuatia hali hiyo ya shehena nyingi kutosafirishwa na kurundikana.

Picha: Yoruk Isik/REUTERS

Mazungumzo ya mjini Istanbul kwa hivyo ambayo ni ya ana kwa ana kati ya maafisa hao wa kijeshi wa Urusi, Ukraine, Uturuki pamoja na Umoja wa Mataifa yatajikita kutafuta njia ya kuwezesha mamilioni ya tani yaliyokwama kwenye maghala kuanza kusafirishwa kutoka bandari za Ukraine kwenye bahari nyeusi  kuelekea bahari ya Mediterenia. Nchi nyingi za ulimwengu unaoendelea na hasa za bara la Afrika zimekuwa katika hali ya kitisho cha kutosambaziwa chakula hali iliyosababisha pia bei ya vyakula kupanda.

Uturuki imeshasema inajitolea kutoa njia salama kwenye bahari nyeusi  na kufanya kazi pamoja na Umoja wa Mataifa, Urusi na Ukraine kufikia makubaliano. Umoja wa Mataifa utaweka kituo mjini Istanbul cha kukagua meli zote.

Bandari nyingi za Ukraine zimefukiwa mabomu na rais wa Urusi Vladmir Putin ameahidi kwamba nchi yake haitotumia njia hizo kuanzisha mashambulizi ikiwa mabomu yaliyotegwa baharini yataondolewa. Ukraine ina mashaka na ahadi ya rais Putin na imemlaumu kwamba vizuizi vyake katika bahari hiyo nyeusi ndivyo vinavyosababisha mizigo kukwama na kusababisha mgogoro wa chakula duniani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW