1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaLibya

Juhudi za kimataifa kuisaidia Libya zashika kasi

Josephat Charo
14 Septemba 2023

Juhudi za kimataifa zimeshika kasi kuisadia Libya kufuatia janga baya kabisa la mafuriko yaliyosababisha vifo vya watu karibu 4,000 na kuwaacha wengine maalfu wakiwa hawajulikani waliko. Vifo huenda vikafikia 20,000.

Hilfsgüter aus Libyen
Picha: Hamza Turkia/Xinhua/picture alliance

Meya wa mji wa Derna, Abdulmenam al-Ghaithi amekiambia kituo cha televisheni cha Al Arabiya jana usiku kwamba wanatarajia idadi kubwa ya wahanga huku vifo vikitarajiwa kufikia kati ya 18,000 na 20,000 mjini humo. Al-Ghaithi amesema mji huo unakabiliwa na janga la kibinadamu kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na kimbunga Daniel. Kauli yake imekuja wakati Umoja wa Mataifa ukisema maalfu ya vifo vingeweza kuepukwa kama mfumo wa tahadhari na usimamizi ungefanya kazi vizuri huku juhudi za kupeleka misaada Libya zikiendelea.

Ndege za kijeshi za kubeba mizigo pamoja na meli kutoka Mashariki ya Kati na mataifa ya Ulaya zimekuwa zikisafirisha misaada ya dharura kwenda nchini Libya. Mbali na watu ambao hawajulikani waliko, maalfu ya wengine wamepoteza makazi yao kufuatia mafuriko yaliyotokea katika mji wa bandari wa Derna.

Jeshi la Ujerumani linapanga kutuma msaada nchini Libya hivi leo. Jeshi hilo limesema ndege zake mbili za mizigo zitaanza safari kutoka uwanja wa ndege wa Wunstorf zikiwa zimebeba mahitaji kama vile magodoro, mahema na majenereta. Serikali ya Ujerumani imeahidi msaada wa haraka kufuatia ombi la Libya kutaka msaada kutoka kwa Umoja wa Ulaya.

Umoja wa Ulaya umeahidi dola milioni 10 kuwasaidia manusura wa mafuriko, wakiwemo watu wapatao 30,000 ambao unasema wameachwa bila makazi katika mji wa Derna. Uingereza nayo imesema inatuma msaada wa thamani ya paundi milioni moja na inashirikiana na washirika wa kuaminika walioko Libya kutambua mahitaji muhimu ya dharura yanayohitajika kama vile makazi, huduma za afya na usafi.

Haki za binadamu zizingatiwe katika utoaji wa misaada

Akizungumzia mafuriko nchini Libya, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu Volker Türk amesema kimbunga Daniel ni tukio lingine linalokumbusha juu ya athari zinazoweza kusababishwa na majanga kwa dunia ambazo zinatokana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Volker Türk, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binadamuPicha: Pierre Albouy/KEYSTONE/picture alliance

Soma pia: Vifo kutokana na mafuriko vyafikia 2,300 Libya

Türk amesema ana huzuni kubwa kwamba maelfu ya maisha yameangamizwa kikatili sana mashariki mwa Libya, na watu wengi zaidi wamepoteza wapendwa wao, nyumba zao, jamii zao, na hawawezi tena kuyafikia mahitaji yao ya kimsingi.

"Nawatolea wito wadau wote wa siasa wa Libya waweke kando mikwamo ya kisiasa na migawanyiko na washirikiane kwa pamoja kuhakikisha misaada inapatikana. Huu ni wakati wa umoja wenye kusudi: wote walioathiriwa lazima wapate msaada bila kuzingatia mafungano yoyote. Ni muhimu kuhakikisha hatua maalum zinachukuliwa ili kuyalinda makundi yanayokabiliwa na hatari - wale waliotumbukia katika hatari zaidi baada ya janga kama hili. Haki za binadamu zipewe kipaumbele katika kuishughulikia hali hii ya kuhuzunisha."

Ujerumani yafuta msaada kwenda Morocco

Kuhusu janga la tetemeko la ardhi nchini Morocco, msaada wa shirika la msalaba mwekundu la Ujerumani uliopangwa kupelekwa kusaidia wahanga wa tetemeko hilo umefutwa dakika ya mwisho.

Katika taarifa yake shirika hilo la Ujerumani limesema kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao na washirika wao Shirika la Msalaba mwekundu na Hilal Nyekundu, sheria na taratibu mpya zimetangazwa katika kipindi kifupi, hali inayoifanya vigumu kwa ndege yao ya misaada kuondoka leo.

Serikali ya Morocco inakabiliwa shinikizo linaloongezeka ikubali msaada zaidi wa kimataifa baada ya kukubali kupokea msaada kutoka kwa nchi chache kama vile Uhispania, Uingereza, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu.

(apa, afp, reuters)

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi