Juhudi za kukabili Ebola zaongezwa Kivu Kusini
22 Mei 2026
Hofu imeongezeka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya mlipuko wa Ebola kuenea hadi jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa Congo eneo linalodhibitiwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda. Haya yanajiri huku juhudi za kimataifa zikielekezwa katika kuongeza ufadhili ili kukabiliana na janga hilo.
Msemaji wa kundi la M23 Lawrence Kanyuka, amesema vipimo vimethibitisha kisa kipya cha Ebola katika eneo la Kabare, Kivu Kusini. Kisa hicho kinamhusu mtu aliyesafiri kutoka mji wa Kisangani mashariki mwa Congo. Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya kimataifa kutokana na kasi ya maambukizi na changamoto za kuudhibiti.
Kwa mujibu wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Umma nchini Congo, watu 160 wanashukiwa kufariki dunia kutokana na Ebola kati ya visa karibu 671 vinavyoshukiwa. Hadi sasa, visa 64 vimethibitishwa rasmi pamoja na vifo sita.
Hata hivyo juhudi za kudhibiti mlipuko huo zimeendelea kukwamishwa na mapigano ya muda mrefu mashariki mwa Congo kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23. Wakati kitovu cha mlipuko huo kiko katika jimbo la Ituri kaskazini mashariki mwa nchi, ambako huduma za afya ni duni na maelfu ya wananchi wamekimbia makazi yao kutokana na machafuko ya makundi yenye silaha.
Afisa mmoja katika kambi ya wakimbizi ya Kigonze amesema hakuna hata sehemu za kunawia mikono kwa zaidi ya wakimbizi elfu kumi na sita waliopo eneo hilo, akionya kuwa mlipuko mkubwa unaweza kusababisha maafa makubwa.
Huku haya yakiarifiwa, ghasia zilizuka katika hospitali ya Rwampara karibu na mji wa Bunia baada ya vijana wenye hasira kuvamia hospitali hiyo na kuchoma mahema ya kutenga wagonjwa wa Ebola.
Mashuhuda walisema umati wa watu ulikusanyika nje ya hospitali ya Rwampara wakidai mwili wa mwanaume aitwaye Elie kabla hali ya taharuki kugeuka kuwa vurugu.
"Tulikuja kumzika mwanangu, kisha tukawaona watu hawa wakija kwa makundi wakidai mwili wa mtu aitwaye Elie. Walianza kurusha mawe na kuchoma moto mahema, na mwili wa mwanangu ukaachwa ukiungua hapo. Sijui nifanye nini. Ukiangalia vizuri utaona mwili ulioungua, huyo ni mwanangu. Tulikuwa tayari tumeandaa jeneza pale, unaona, lakini haya mambo ya Ebola ni magumu sana.”
Mhudumu mmoja wa afya alijeruhiwa kwa kupigwa mawe kabla ya vikosi vya usalama kuingilia kati.
Hatua za Kimataifa
Mamlaka zimeimarisha ukaguzi wa afya katika viwanja vya ndege huku Shirika la Afya Duniani pamoja na mashirika ya misaada yakipeleka tani za vifaa vya matibabu katika maeneo yaliyoathirika.
Umoja wa Mataifa umetoa takribani dola milioni 60 kutoka katika mfuko wa dharura kusaidia kudhibiti mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na kupeleka wafanyakazi zaidi huku Norway ikisema itachangia milioni 50 za Norway sawa na dola milioni 5.41 za Marekani katika mfuko wa dharura wa Shirika la Afya Duniani.
Ingawa WHO inaeleza kuwa hatari ya kuenea kwa Ebola kimataifa bado ni ndogo, nchi mbalimbali zimeanza kuchukua tahadhari zaidi. Mamlaka ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani imesema ndege ya Air France iliyokuwa ikielekea Detroit ilielekezwa kutua Montreal baada ya abiria kutoka Congo kupanda ndege mjini Paris "kimakosa” huku kukiwa na vikwazo vya safari.
Msemaji wa taasisi hiyo alisema abiria huyo "hakupaswa kupanda” ndege hiyo Jumatano kutokana na masharti ya Marekani ya kuingia nchini yaliyowekwa ili kupunguza hatari ya kuenea kwa Ebola.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya nchini Uganda, Diana Atwine, amesema katika taarifa iliyotolewa Kampala kuwa Kikosi Kazi cha Taifa (NTF), kinachoongozwa na Makamu wa Rais Jessica Alupo, kimeamua kusimamisha safari zote za ndege kati ya Uganda na DRC, huku hatua hiyo ikitarajiwa kuanza kutekelezwa ndani ya saa 48.