1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuunga mkono uhuru wa habari zapungua duniani

Angela Mdungu
3 Mei 2024

Shirika linalotetea waandishi wa habari la 'Reporters Without Borders' limetahadharisha kuhusu kuporomoka kwa juhudi za serikali kuunga mkono uhuru wa vyombo vya habari ulimwenguni.

Pakisten I Presse - Supreme Court in Islamabad
Picha: Aamir Qureshi/AFP/Getty Images

Shirika hilo la kutetea haki za waandishi wa habari katika ripoti yake ya mwaka limetoa tahadhari kuwa serikali zimekuwa zikipunguza kasi ya kuunga mkono uhuru wa habari.

Maelezo hayo yametolewa katika ripoti ya mwaka ya takwimu za uhuru wa vyombo vya habari za mwaka. Kulingana na takwimu za shirika hilo Norway imeendelea kuwa ya kwanza kwa kuwa na uhuru wa habari, wakati Eritrea ikikamata nafasi ya mwisho.  Katika ripoti hiyo mataifa yaliyotajwa kuporomoka kwa kiasi kikubwa katika uhuru wa habari ni  Afghanistan, Togo na Equador.

Taarifa hiyo ya hali ya uhuru wa habari imetolewa ikiwa ni siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kusema kuwa siku ya Umoja wa Mataifa ya Uhuru wa habari ni muhimu sana na kutoa wito kwa serikali, sekta binafsi na asasi za kiraia kuhakikisha kuwa kuna dhamira ya dhati ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari na haki za waandishi na wanahabari kote duniani.

DW yamtunuku Yulia Navalnaya tuzo ya uhuru wa habari

Kwingineko, shirika la habari la kimataifa la DW leo limemtangaza Yulia Navalnaya na wakfu wa Alexei Navalny wa kupambana na rushwa kuwa washindi wa tuzo ya kumi ya uhuru wa habari. Navalnaya ni mjane wa aliyekuwa kiongozi wa upinzani wa Urusi Alexei Navalny.

Soma zaidi: Dunia yaadhimisha uhuru wa vyombo vya habari

Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa DW Peter Limbourg amesema kuwa Yulia Navalnaya ameunga mkono juhudi za mumewe  za kisiasa katika kupigania uhuru wa habari na wa kujieleza nchini Urusi.  Atakabidhiwa rasmi tuzo hiyo Juni 5 mjini Berlin.

Yulia NavalnayaPicha: Johanna Geron/REUTERS

Nalo Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO limewatunuku tuzo ya uhuru wa habari waandishi wa habari wa Kipalestina. Mkurugenzi wa shirika hilo  Audrey Azoulay amesema tuzo hizo kwa mwaka huu zimetolewa kuwapa heshima waandishi wa habari wenye ujasiri na wanaofanya kazi katika mazingira hatari.

Kulingana na kamati maalumu ya kuwalinda waandishi ya Marekani ya CPJ, Takriban waandishi wa habari 97 na wafanyakazi wa vyombo vya habari wameuwawa tangu vita kati ya Israel na kundi la Hamas vilipoanza katika Ukanda wa Gaza.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW