1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuufumbua mzozo nchini Mali

29 Machi 2012

Viongozi wa kijeshi wa Mali wanazidi kushinikizwa warejee kambini, huku rais aliyepinduliwa Amadou Toumani Toure,akijitokeza kwa mara ya kwanza na kusema yu salama.Na viongozi wa ECOWAS wanakwenda Bamako.

Rais liyepinduliwa wa Mali Amadou Toumani TourePicha: AP

Katika wakati ambapo dalili za kupatikana maridhiano kati ya viongozi wa Afrika magharibi na viongozi wa kijeshi nchini Mali zinazidi kuchomoza,rais aliyepinduliwa na wanajeshi March 22,Amadou Toumani Touré anasema yuko salama mjini Bamako na hajafungwa.Katika mahojiano ya muda mfupi ya simu pamoja na shirika la habari la Ufaransa AFP , rais Amadou Toumani Toure ambae hakuna aliyemsikia tangu wanajeshi waliponyakuwa madaraka,amesema yeye na familia yake wako katika hali nzuri.Hakutaka lakini kusema yuko wapi hasa, akisisitiza hilo si muhimu.Anasema anafuatilizia yote yanayotokea na kuongeza:"Anaunga mkono moja kwa moja mapendekezo yaliytolewa na viongozi ili kuupatia ufumbuzi mzozo nchini .Miezi miwili kabla ya mhula wake kumalizika,anasema yuko tayari kuridhia ufumbuzi wa aina yoyote utakaoleta utulivu na kuhifadhi demokrasia  nchini Mali inayojivunia sifa nzuri".

Hatima yake ilizusha dhana kama anashikiliwa na wanajeshi waliompinduwa au analindwa na wanajeshi wanaomtii.

Mkuu wa utawala wa kijeshi kepteni Amadou Sanogo na Ufaransa,walijaribu hapo awali kutuliza hofu hizo,bila ya kutoa lakini maelezo zaidi.

Maandamano ya wafuasi wa utawala wa kijeshi mjini BamakoPicha: Reuters

Takriban vyama vyote vya kisiasa,vinaupinga utawala wa kijeshi.Kimoja tu,chama cha mshikamano wa kiafrika kwaajili ya Demokrasia na uhuru-SADI ndicho kinachounga mkono utawala wa kijeshi.Wao ndio walioitisha maandamano  kuunga mkono utwala huo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Bourkina Fasso Djibril Bassolé amezungumzia uwezekano wa kufikiwa maridhiano.

Viongozi wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi Afrika magharibi-ECOWAS wanazungumzia "kipindi cha mpito ambacho kingeongozwa na spika wa bunge lililovunjwa na wanajeshi-Dioncounda Traoré.

Rais Allasane Ouattara wa Côte d'Ivoire (kati kati) ataongoza ujumbe wa Ecowas nchini MaliPicha: Reuters

Ujumbe wa viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi unaoongozwa na rais Allassane Ouattara wa Côte d'Ivoire,mwenyekiti wa zamu wa ECOWAS unatarajiwa kuwasili Bamako leo kwa mazungumzo pamoja na viongozi wa kijeshi kwa lengo la kurejesha nidhamu na utawala unaoheshimu sheria.

Ziara hiyo imetanguliwa na ile ya wakuu wa kijeshi wa jumuia ya ECOWAS ambao walikuwa na mazungumzo pamoja na watawala wa kijeshi.Mkuu wa vikosi vya wanajeshi vya Côte d'Ivoire,Soumaila Bakayoko amesema "wamewasili risala za maana."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW