1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kuunusuru Umoja wa Ulaya Magazetini

Oumilkheir Hamidou
6 Machi 2019

Juhudi za kuunusuru Umoja wa Ulaya usidhibitiwe na vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na uamuzi wa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw kuwafuta vigogo watatu wa timu bingwa ya Bayern Munich Magazetini

Frankreich - Präsident Macron - Europa
Picha: picture-alliance/AP/G. Vanden Wijngaert

Tunaanza na juhudi za kuuokoa Umoja wa ulaya. Gazeti la "Mannheimer Morgen "linaandika: "Katika mataifa wanachama wa umoja wa Ulaya zimeibuka hisia za kuunga mkono Umoja wa ulaya, lakini hisia hizo hazitoshi ikiwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na vile vinavyopigania uzalendo ndivyo vinavyowahimiza wafuasi wao. Wapiga kura wanaweza kujifunza kwa kuchukua mifano ya Uingereza na Marekani na kutambua kupinga kitu pekee haitoshi, watu wanabidi wapaze sauti ikilazimika na kupania kwaajili ya kile wanachokipigania.

Mbinu za Macron zinaweza kuleta tija

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameonyesha mfano, linaandika gazeti la mji mkuu "Berliner Morgenpost": "Rais wa Ufaransa ameifungua kwa kishindo kampeni ya uchaguzi wa Ulaya. Anajitambulisha kuwa kiongozi wa vuguvugu linalopigania Umoja wa Ulaya ulio huru, wa kidemokrasi na wa mshikamano dhidi ya wale wanaotaka kuuona Umoja wa Ulaya unageuka kuwa wa siasa kali za kizalendo. Katika nchi nyingi za Umoja wa Ulaya hofu zimeenea wafuasi wa siasa kali za kizalendo wasije wakapata nguvu uchaguzi wa bunge la Ulaya utakapoitishwa mwezi May unaokuja.

Macro anataka kuziondowa hofu hizo kwa kupendekeza yale yale  yaliyompatia ushindi uchaguzi wa rais ulipoitishwa nchini Ufaransa mwaka 2017. Jamii inabidi iutambue na kuupanua uwezo wake  na kipaji chake . Ikiwa mjadala utafuata mkondo huo basi Emmanuel Macron anaweza kulifikia lengo lake."

Sera ya Ujerumani kuelekea Umoja wa Ulaya

Gazeti la kusini magharibi "Stuttgarter Nachrichten" linakosoa sera ya Ujerumani kuelekea Umoja wa Ulaya na kuandika: "Watu wangependelea kuona sera ya Ujerumani inajihusisha zaidi na mjadala na sio tu kuzungumzia ratiba za uchaguzi wa Ulaya au kukariri mapendekezo yaliyotolewa na wadau wengine wa Umoja wa Ulaya. Hata kama kuna sababu za kihistoria za hali hiyo kwamba Ujerumani haipaswi kupaza sauti barani Ulaya, hata hivyo kuna umuhimu kuona sauti ya Ujerumani pia inasikika. Mjadala kuhusu mageuzi ya Umoja wa Ulaya utaleta tija pia nchini Ujerumani badala ya kampeni chapwa ya uchaguzi wa Ulaya."

Uamuzi jasiri wa Joachim Löw

Hatimae wahariri wamesifu moyo wa kijasiri wa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw aliyeamua kuwafuta vigogo watatu wa timu bingwa wa mabingwa, Bayern Munich toka orodha ya wanasoka wa timu ya taifa "die Mannschaft". Gazeti la Südkurier" linaandika: "Kwa muda mrefu Joachim Löw alikuwa akikosolewa eti hana analolifanya. Muda mrefu umepita tangu pigo lililosababishwa na kutolewa kwa aibu timu ya taifa ya Ujerumani katika kombe la dunia, Joachim Löw hakupitisha uamuzi wowote. Sasa lakini amepiga moyo konde. Kwasababu unahitaji moyo wa kijasiri kuweza kuwatoa vigogo wa timu ya Bayern Munich Müller, Boateng na Hummels toka timu ya taifa. Hata kama uamuzi huo kimchezo ni wa busara. Atakaefuata atakuwa mlinzi wa lango la timu ya taifa Manuel Neuer."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW