Juhudi za upatanishi za Wapalestina zatarajiwa kufanikiwa
6 Oktoba 2017Waziri mkuu wa Palestina Rami Hamdallah aliwasili katika mji wa Gaza kwa mara ya kwanza tangu mwaka wa 2015, akieleza kuwa huo ni wakati wa "kihistoria."
Alikutana na viongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniya, pamoja na mkuu wa upelelezi wa Misri pamoja na baraza la mawaziri kwa mara ya kwanza baada ya karibu ya miaka mitatu. Kundi hilo la Hamas lilitawala eneo la Gaza tangu mwaka wa 2007, tangu ilipouchukua mikononi mwa serikali ya mamlaka ya Palestina katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na kufeli kwa majaribio mengi ya awali ya upatanishi.
Lakini baada ya juhudi za upatanishi za Misri, mwezi uliopita, kundi la Hamas lilikubali kuirudishia mamlaka serikali inayotambulika kimataifa ambayo makao yake makuu yako Ukingo wa magharibi.
Miongoni mwa mambo muhimu yanayostahili kujadiliwa ni hali ya wakaazi millioni mbili walioko gaza ambao wamekumbana na vita vitatu vibaya zaidi na Israel tangu mwaka wa 2008, pamoja na kuwekewa vikwazo na Israel na Misri. Wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa umeme na ukosefu mkubwa wa ajira. Mgawanyiko wa miaka kumi wa Palestina pia umekuwa kikwazo kwa mazungumzo ya amani na Israel.
Pande hizo mbili zinatakiwa kuunda taifa litakalojitegemea lakini rais anayetambulika kimataifa Mahmud Abbas, mshirika wa muda mrefu wa mazungumzo na Israeli, amehujumiwa na udhibiti wa Gaza chini ya kundi la Hamas.
"Mgawanyiko huu unawazuia Wapalestina kuweza kujipanga ikatika kufikia lengo la kurudi kwenye mazungumzo na kupelekea kupatikana kwa suluhisho," mjumbe wa Umoja wa Mataifa ya Mashariki Kati Nickolay Mladenov aliiambia shirika la habari la AFP.
Juhudi za awali ambazo zilifeli zimeibua shaka juu ya kufanikiwa kwa jitihada hizi za sasa za upatanishi.
Lakini safari hii matumaini yapo hasa baada ya mawaziri kukutana na waziri mkuu wa serikali ya Palestina mjini Gaza kinyume na hapo awali.
Ikiwa ziara ya wiki hii ni ishara ya mafanikio basi, wiki ijayo majadiliano yanaanza.
Pande hizo mbili zitakutana mjini Cairo jumanne wiki ijayo kuanza majadiliano ya kina ambayo yanaweza kuchukua miezi. Kikwazo kikubwa ni udhibiti wa usalama katika mji wa Gaza. Hamas na tawi la kijeshi na linalokadiriwa kuwa na wanachama 25,000 na halifurahishwi na hatua ya kukabidhi mamlaka kwa Abbas jambo ambalo kiongozi huyo amelisisitizia kuwa ndiyo sharti kuu.
Hatua ya pili muhimu katika majadiliano itakuwa hatima ya maelfu ya wafanyakazi wa serikali walioajiriwa na Hamas tangu 2007. Je, serikali ya Palestina itawajumuisha kwenye safu zake?
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu tayari ameonya kuwa serikali yake haitakubali mpango wowote wa upatanishi hadi kundi la Hamas itakaposalimisha silaha na kutambua haki ya kuwepo kwa dola ya Israeli. Marekani ambayo inataka kuanzisha upya mchakato wa amani wa Israeli na Palestina, imezikaribisha juhudi zinazofanyika hivi sasa miongoni mwa wapalestina .
Mwandishi: Fathiya Omar/APE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman