1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi zafanyika kuwazuia mafisadi kugombea nchini Kenya

Daniel Gakuba
18 Mei 2022

Wadau wa kukabiliana na ufisadi nchini Kenya wanatafuta mbinu za kuwazuia wanasiasa ambao uadilifu wao unatiliwa shaka, kuwania nyadhifa kwenye uchaguzi mkuu ujao. Je, watafua dafu?

Sudan Wahlen 2010
Picha: AP

Tume ya uchaguzi nchini IEBC, inapojiandaa kwa awamu inayofuata ya mchakato wa uchaguzi mkuu ujao, wadau wanaikosoa tume hiyo kwa kutozingatia kipengee cha maadili kwenye katiba kwa kuwaruhusu wagombea ambao maadili yao yanatiliwa shaka.

Mkurugenzi wa tume ya kukabiliana na ufisadi humu nchini, EACC, Twali Mbarak amesema wanatafuta mbinu za kuhakikisha kwamba wanasiasa ambao uadilifu wao unatiliwa shaka wanazuiwa kuwania nyadhifa kwenye uchaguzi mkuu.

Soma Zaidi: Changamoto za kiusalama kuhusu uchaguzi Kenya

Mbarak anaeleza kwamba wamejaribu kuwazuia viongozi walio na ukosefu wa maadili kuwania viti, lakini juhudi zao zimekuwa zikigonga mwamba kwa kuwa viongozi hao wametumia mianya iliyoko kwenye sheria kuingia kwenye uongozi wa ofisi za umma.

Wanaharakati wanataka wagombea wa kisiasa nchini Kenya wawe waadilifuPicha: picture-alliance/ dpa

IEBC yatofautiana na ofisi ya mashitaka

Tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi nchini Kenya na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Hajj, imesema haitabadili msimamo wake ambao unatofautiana na IEBC inayosema viongozi wa kisiasa walio na kesi mahakamani bado hawana hatia kwa hiyo wako huru kuwania nafasi mbalimbali za siasa.

Hii ni kutokana na uamuzi wa mahakama kuu uliotolewa majuma mawili yaliyopita iliyoagiza kwamba kamati ya IEBC inayoshughulikia uchaguzi ni kinyume na sheria.

Soma zaidi: Tume ya uchaguzi Kenya yashindwa kufikia malengo ya usajili

Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani na mwanaharakati Okiya Omutata aliyetaka mahakama itangaze kwamba IEBC ina uwezo wa kumzuia mtu asiye na maadili au kuhusishwa na ufisadi kuwania nafasi ya kisiasa kulingana na katiba.

Kampeni za kisiasa nchini Kenya hujaa uchangamfuPicha: picture-alliance/ dpa

Tume hiyo imesema ni jukumu lake kuidhinisha sheria za uchaguzi, lakini uamuzi wa mahakama uliotolewa umewazuia kuzitekeleza sheria hizi.

Raslimali ni kikwazo katika kupambana na mafisadi

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Noordin Hajj amesema ofisi yake inatekeleza mchakato wakizingatia changamoto ambazo huenda zikajitokeza kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Soma zaidi: Mchakato wa marekebisho ya katiba Kenya waanza

''Kile ambacho tunafanya kama ofisi ya mashtaka, ni kutenga rasilimali, wataalam na uwezo wetu kuhakikisha kwamba tunazingatia mahitaji ya uchaguzi mkuu nchini Kenya. Na kwamba vurugu na matumizi mabaya ya mamlaka hayashuhudiwi wakati huu.'' Amesema.

Pamoja na kuhakikisha sura ya sita ya katiba ya Kenya inatekelezwa kikamilifu, wadau hawa wamesisitiza kwamba watashinikiza kuwepo kwa haki na usawa katika uchaguzi mkuu ujao.

 

Mwandishi: Wakio Mbogho/DW Nakuru

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW