1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUturuki

Juhudi zahamia kwenye mzozo wa kibinadamu Uturuki-Syria

14 Februari 2023

Waokoaji wameanza kuhitimisha utafutaji wa manusura nchini Uturuki na Syria, huku juhudi zikielekezwa kwenye kuwasaidia wahanga wa tetemeko kubwa la ardhi ambalo limesababisha vifo vya zaidi ya watu 35,000.

Türkei Nurdagi | Rettungsarbeiten nach Erdbeben
Picha: Chris McGrath/Getty Images

Syria, ambayo tayari imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka 12, inatia wasiwasi sana. Umoja wa Mataifa ulifanya mkutano wa dharura jana Jumatatu kuhusu jinsi ya kuongeza msaada kwa maeneo yanayodhibitiwa na waasi, huku hasira ikiongezeka kutokana na mwitikio wa kujikongoja wa kimataifa kwa taifa hilo lililotengwa.

Rais wa Syria Bashar al-Assad, aliyetengwa na kuwekewa vikwazo na mataifa ya Magharib, alitoa wito wa msaada wa kimataifa kusaidia kujenga upya miundombinu nchini humo, ambapo Umoja wa Mataifa unakadiria watu zaidi ya milioni tano wameachwa bila makazi.

Soma pia: UN:Juhudi za uokozi Uturuki na Syria zakaribia mwisho

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Assad amekubali kufungua vivuko viwili zaidi vya mpakani -- Bab Al-Salam na Al Raee kutoka  Uturuki hadi kaskazini magharibi mwa Syria -- ili kuruhusu misaada.

Kabla ya tetemeko la ardhi kutokea, karibu misaada yote muhimu ya kibinadamu kwa zaidi ya watu milioni nne wanaoishi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kaskazini magharibi mwa Syria ilikuwa ikitolewa kutoka Uturuki kupitia kivuko cha Bab al-Hawa.

Rais wa Syria Bashar al-Assad akiwa katika mazungumzo na mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffith mjini Damascus, Februari 13, 2023.Picha: Syrian Presidency/Facebook/AP Photo/picture alliance

Guterres alisema kufungua vivuko hivyo pamoja na kuwezesha njia za kibinadamu, kuharakisha uidhinishaji wa viza na kurahisisha usafiri kati ya vituo, kutaruhusu misaada zaidi kuingi kwa haraka.

Siku nane baada ya tetemeko hilo la ukubwa wa 7.8 kupelekea majengo kubomoka katika eneo lote, simulizi zinaendelea kuibuka za watu waliopatikana wakiwa hai kwenye vifusi, lakini wataalam wanaonya kuwa matumaini ya kunusurika yanafifia.

Soma pia: Majengo ya zamani, matetemeko madogo yalisababisha zahma Uturuki na Syria

Nchini Uturuki Jumatatu, watoto ndugu, Harun mwenye umir wa miaka 8 na Eyuphan wa miaka 15, waliokolewa masaa 181 tangu kutokea kwa tetemeko hilo ambalo ni la tano kwa ukubwa katika karne hii ya 21, liliripoti shirika la habari la Anadolu.

Idadi ya vifo iliyothibitishwa imefikia 35,331 huku maafisa na matabibu wakisema watu 31,643 wamekufa nchini Uturuki na wasioungua 3,688 nchini Syria. Manusura wanakabiliwa na ukosefu wa maji na vyoo duni.

Katika eneo la Adiyaman kusini mwa Uturuki, kumeripotiwa mlipuko wa upele, ambao ni ugonjwa wa ngozi unaojulikana kuenea katika maeneo yenye watu wengi, ukiwaathiri watu wazima, wakati watoto wakikabiliwa na maradhi ya kuharisha.

Watu wakipumzika wakati utafutaji wa manusura ukiendelea kufuatia tetemeko kubwa la ardhi mjini Kahramanmaras, Uturuki, Februari 12, 2023.Picha: Suhaib Salem/REUTERS

Makamu wa Rais wa Uturuki Fuat Oktay alisema watoto 574 waliotolewa kwenye majengo yaliyoporomoka walipatikana bila wazazi walionusurika, na 76 pekee ndiyo wamekabidhiwa kwa wanafamilia wengine. Chama cha waajiri nchini Uturuki kimeripoti jana kuwa gharaza za janga hilo zinaweza kufikia dola bilioni 84.1.

Soma pia:Erdogan atangaza hali ya dharura katika maeneo ya tetemeko 

Nchini Syria, idadi ya vifo haijabadilika pakubwa kwa siku kadhaa sasa na inatarajiwa kuongezeka. Mkuu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffith, alitarajiwa kutoa maelezo mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya nchini Syria, baada ya kuzuru kanda hiyo mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni, Tedros Adhanom Ghebreyesus, alisema Damascus ilitoa idhini kwa misafara ya misaada kutoka maeneo ya serikali, lakini WHO ilikuwa bado inasubiri ruhusa kutoka maeneo yanayodhibitiwa na waasi kabla ya kuingia.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW