1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi zaidi za kidiplomasia zaendelea kutaka mkataba wa kusitisha mapigano kati ya Israel na Palestina

Aboubakary Jumaa Liongo5 Februari 2009

Mjumbe wa Israel, Amos Gilad anatarajiwa kuwasili mjini Cairo Misri hii leo, ikiwa ni baada ya kundi Hamas kutaka ufafanuzi zaidi kuhusiana na nafasi ya Israel katika makubaliano ya makubaliano ya kusitisha mapigano

Wanajeshi wa Israel wakiwa katika doria kwenye mpaka wa nchi hiyo na Ukanda wa GazaPicha: AP

Mjumbe huyo wa Israel anatarajiwa kuwa na mazungumzo na mpatanishi wa Misri Omar Suleiman na kujibu maswali yaliyowasilishwa na Hamas juu mkataba huo pamoja na kuondolewa kwa vizuizi vya kuingia na kutoka Ukanda wa Gaza.


Mjumbe huyo wa Israel amekuwa akienda mara kadhaa nchini Misri katika juhudi za kidiplomasia kutafuta mkataba wa kusitisha mashambulizi kati ya Israel na Palestina, ambapo mara ya mwisho ilikuwa tarehe 22 mwezi uliopita.


Hapo jana ujumbe wa Hamas uliondoka Cairo bila ya kufikiwa kwa makubaliano ya muda mrefu ya kusitisha mashambulizi kati ya pande hizo mbili, ukidai ya kwamba kuna masuala kadhaa yanahitaji ufafanuzi hususan kuhusiana na kufunguliwa kwa mpaka na kuingia kwenye eneo la pwani ya Gaza.


Mohamed Nasri ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Hamas katika mazungumzo hayo akizungumza na shirika la habari la AFP amesema kuwa Israel inajaribu kukwepa kuufungua mpaka wake na Gaza.


Amesema kuwa Hamas wanategemea kupata majibu ya maswali yao kutoka kwa mpatanishi wa Misri ambaye anakutana na mjumbe wa Israel.


Hamas wamesema kuwa wako tayari kutekeleza mkataba wa kutoshambuliana na Israel kwa muda wa mwaka  mzima lakini iwapo Israel itaufungua mpaka wake na Gaza kikamilifu.


Ikumbukwe ya kwamba makubalino ya awali ya kutoshambulia kwa miezi sita yalikuwa ni makubalino ya mdomo tu na si ya maandishi.


Ujumbe huo wa Hamas uliondoka jana Cairo na haukutoa tarehe kamili ya lini waterejea tena Misri kuchukua majibu ya maswali yao.


Huko Gaza msemaji wa Hamas Fawzi Barhum ameilaumu Israel kuwa inataka kuliunganisha suala la kuondolewa kwa vizuizi ilivyoweka na kuachiwa huru kwa mwanajeshi wake koplo Gilad Shalit ambaye alitekwa na wanamgambo wa kiislam huko Gaza June 2006.


Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi wa Israeli Ehud Barak amesema kuwa meli za kijeshi za nchi hiyo zimeizuia meli moja iliyokuwa imebeba  misaada ya kibinaadamu kutoka Lebanon kwenda Ukanda wa Gaza.


Waziri huyo wa Ulinzi wa Israel amesema kuwa meli hiyo imepelekwa kwenye bandari ya Ashdod nchini Israel. Meli hiyo iliwasili jana huko Ukanda wa Gaza katika kile kinachoonekana kupuuza hatua ya Israel kuweka vizuizi kuingia Ukanda wa Gaza kwa njia zote za majini na nchi kavu.


Waandishi wa habari wa vituo vya televisheni za kiarabu vya Al-Jadeed na Al-Jazeera ambao walikuwa miongoni mwa watu katika meli hiyo wamesema kuwa meli za Israel ziliifyatulia risasi meli hiyo iitwayo Brotherhood Ship, kabla ya wanajeshi kuivamia na kuingia ndani ambapo waliwapiga mabaharia.


Wamesema kuwa hawakuweza kurusha picha za tukio hilo, baada ya wanajeshi hao wa Israel kuchukua vifaa vyao vya kazi. Hata hivyo jeshi la Israel limekanusha kuishambulia na kuwapiga mabahari hao.


Meli hiyo ilikuwa na watu 18 akiwemo kasisi mmoja wa kigiriki mwenye umri wa miaka 86, ambapo jeshi la Israel limesema kuwa huenda watu hao wakakabidhiwa kwa polisi wa nchi hiyo.


Katika hatua nyingine vikosi vya Israel vimempiga risasi na kumuua mpiganaji mmoja wa kipalestina nyumbani kwake huko Ukingo wa Magharibi.


Msemaji wa jeshi la Israel amesema kuwa mpiganaji huyo Al´a Abu al-Rob mwenye umri wa miaka 23 ni wa kundi la wapiganaji wa kiislam la Islamic Jihad na anashukiwa kuhusika na mashambulizi kadhaa dhidi ya Waisrael.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW