1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jukwaa la Davos laanza

16 Januari 2023

Kongamano linalojadili hali ya uchumi duniani linaanza katika mjini Davos, huku uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine ukitawala mazugumzo kutokana na athari mbaya kwa sekta ya nishati na upatikanaji wa chakula ulimwenguni

WWF Davos 2023 Auftakt
Picha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Jukwaa la Uchumi Duniani ambalo linahudhuriwa na wanasiasa, wafanyabiashara, watu mashuhuri na wanaharakati wakubwa wa masuala ya kijamii - maarufu kama jukwaa la Davos - lilianza Jumatatu (Januari 16) katika mji wa milima ya Alpen nchini Uswisi. 

Kongamano hilo linafanyika wakati dunia ikiwa kwenye mfadhaiko mkubwa unaodhihirika kupitia mfumko mkubwa wa bei za bidhaa muhimu, mgogoro wa nishati na kuharibika kwa mfumo wa usambazaji bidhaa duniani kulikosababishwa na vita nchini Ukraine na kuzuka upya kwa maambukizo ya virusi vya korona nchini China.

Mwanzilishi wa jukwaa hilo, Klaus Schwab, aliwaambia waandishi wa habari kwamba dunia ipo kwenye mkwamo ambao lazima viongozi wa dunia waukwamue.

Soma zaidi: Matajiri waomba kutozwa kodi

"Migogoro ya kiuchumi, kimazingira, kijamii na siasa za kilimwengu inazidi kutanuka na kujichwanya, huku ikiandaa mustakabali mgumu sana na usio na uhakika. Mkutano huu wa kila mwaka wa Davos lazima ujaribu kuhakikisha kuwa viongozi hawasalii kunasa kwenye akili hii ya migogoro." Alisema Schwab.

Viongozi kutoka mataifa 50 wahudhuria

Mkutano huo wa siku tano ambao kauli yake mbiu ni "Ushirikiano kwenye Dunia iliyoparaganyika" ulitazamiwa kushuhudia wakuu wa nchi na serikali wapatao 50 wakishiriki. Miongoni mwao ni Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani, Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen, na Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez.

Marekani itawakilishwa na mjumbe maalum wa mabadiliko ya tabia nchi, John Kerry, na mwakilishi wake wa biashara, Katherine Tai.

Muasisi wa Jukwaa la Uchumi Duniani, Klaus Schwab.Picha: Laurent Gillieron/KEYSTONE/dpa/picture alliance

Nchi tajiri kiuchumi zatakiwa kupunguza umasikini duniani

02:02

This browser does not support the video element.

Lakini Urusi, hasimu mkubwa wa Marekani, haitahudhuria kwani Jukwaa hilo lilisitisha mahusiano yake na nchi hiyo tangu Moscow kuivamia Ukraine Februari mwaka jana.

Ramaphosa, Samia kuongoza ujumbe wa Afrika

Viongozi waliochaguliwa hivi karibuni, akiwemo Rais Yook Suk Yeol wa Korea Kusini, Gustavo Petro wa Colombia na Ferdinand Marcos Jr. wa Ufilipino pia watahudhuria. Bara la Afrika linatazamiwa kuongozwa na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini na Samia Suluhu Hassan wa Tanzania.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania anaongoza ujumbe wa Afrika kwenye kongamano hilo akiwa na mwenzake wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.Picha: Ericky Boniphace/DW

Afrika inatekeleza kwa sasa Mradi mkubwa kabisa wa biashara na soko huria ulimwenguni, ambao kama ukifanikiwa utaunda nafasi milioni 30 za ajira.

Soma zaidi: Davos: Kongamano la uchumi wa dunia lamalizika

Rais wa jukwaa hilo, Borge Brende, alisema mkutano wa mara hii unafanyika wakati wa mzozo mkubwa wa kilimwengu lakini ni alama muhimu kwa bara la Afrika.

"Hakuna shaka kwamba mkutano wetu wa 53 wa kila mwaka hapa Davos unafanyika wakati kukiwa na hali ngumu saa kwenye siasa na uchumi wa ulimwengu. Kuna mengi yaliyo hatarini panapohusika uchumi wa dunia, ambayo yanatutaka tuhakikishe tunaepuka mserereko wa uchumi, ukuwaji mdogo, ukosefu wa nishati na kupanda kwa bei ya chakula."Alisema Brende.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW