Jukwaa la Uchumi Duniani lafunguliwa Davos
20 Januari 2026
Kitisho chake cha kuyawekea mataifa ya Ulaya ushuru kwa kupinga azma yake ya kutaka kuitwaa Greenland, kinatarajiwa kuwa mojawapo ya ajenda kuu katika jukwaa hilo.
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Bessent Jumanne alielezea matumaini kuwa Marekani na nchi za Ulaya zitapata suluhu kuhusiana na lengo la Marekani la kuitwaa Greenland, akipuuza madai ya kuzuka kwa vita vya kibiashara.
"Ni saa 48 tu zilizopita. Kama nilivyosema, tulieni tu. Nina imani kuwa viongozi hawatoifanya hali hii kuwa mbaya zaidi na hili litaishia kwa njia itakayomridhisha kila mmoja kwa usalama wa kitaifa wa Marekani na Ulaya," alisema Bessent.
Ushuru kwa bidhaa za Ulaya
Rais Trump amerejelea kusisitiza kuwa hatokubali chochote kile isipokuwa Marekani kuimiliki Greenland, ambayo ni sehemu ya Denmark yenye utawala wa ndani. Lakini viongozi wa Denmark na Greenland wote wamesisitiza kuwa kisiwa hicho hakiuzwi na kwamba hawataki kuwa sehemu ya Marekani.
Jumamosi iliyopita Trump alitangaza ushuru kwa bidhaa za mataifa ya Ulaya yanayoupinga huo mpango wake. Mataifa ya Ulaya yanasema hatua hiyo inakiuka makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa mwaka jana.
Mnamo siku ya Alhamis viongozi wa Ulaya wanatarajiwa kujadiliana njia za kukijibu kitisho hicho cha Trump katika mkutano wa dharura wa kilele mjini Brussels. Huenda wakaziwekea bidhaa za Marekani ushuru wa dola bilioni 108 kuanzia Februari 6.
Huku Trump akitarajiwa kuhudhuria na kutoa hotuba yake kesho, Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Ursula von der Leyen na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanatarajiwa kutoa hotuba zao mbele ya jukwaa hilo la uchumi, Jumanne.
Wataungana na Naibu Waziri Mkuu wa China He Lifeng na Waziri Mkuu wa Canada Mark Carney ambao serikali zao ziko kwenye mivutano na Trump.
Merz kufanya mkutano na Trump
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz anatarajiwa kukutana na kufanya mkutano na Trump Jumatano huko Davos, na amewaambia waandishi wa habari kuwa anatarajia kulijadili suala la Greenland na kiongozi huyo wa Marekani.
"Hatutaki hali izidi kuwa mbaya, hatutaki mzozo huu wa kibiashara na Marekani, ila tukiwekewa ushuru ambao tunaona haufai, basi tutajibu. Na mimi nataka tupate mwafaka," alisema Merz.
Merz lakini amesema hajapuuza tahadhari za Trump kuhusiana na umuhimu wa kimkakati wa Greenland na haja ya kuilinda. Ingawa amesema wakati mmoja wa Vita Baridi, Marekani ilikuwa na zaidi ya wanajeshi 30,000 Greenland, ila wakaviondoa vikosi hivyo.
Vyanzo: Reuters/DW/AP