Jukwaa la utawala wa mtandao wa intaneti lafanyika Tanzania
30 Mei 2025
Hayo yameelezwa Ijumaa (30.05.2025) katika ufunguzi wa jukwaa la 14 la utawala wa mtandao wa intaneti ambako wawakilishi zaidi ya 2000 kutoka nchi za Afrika wamekutana.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa jukwaa hilo, Waziri wa Sayansi na teknolojia, wa Tanzania, Jerry Silaa pamoja na mambo mengine, amesisitiza umuhimu wa sauti za vijana katika ulimwengu wa intaneti.
"Kwa wavumbuzi wadogo, watunga sera wachanga na watumiaji vijana wa mtandao wa intaneti, sauti zenu ni muhimu katika wakati huu wa mabadiliko ya teknolojia, uvubiifu wenu ni muhimu, na jukwaa hili linatakiwa kutumika kama sehemu ya mabadiliko kwa ukuaji wenu na kwa manufaa ya taifa", alisema Silaa.
Kadhalika Waziri, Silaa ametaja mikakati iliyofanywa na serikali ya Tanzania katika kuwekeza kwenye teknolojia ya habari na mawasiliano na kuieleza hadhira hiyo kuwa serikali imewekeza katika Uchumi wa kidijitali, mtandao na kufungua taasisi kadhaa zinazosimamia ithibati ya teknolojia ya TEHAMA.
Katika jukwaa hilo ambalo kwa mwaka huu kauli mbiu ni ‘kuwezesha mustakabali wa dijitali Afrika, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Alhagie Mbow ambaye pia ni mbunge katika bunge la Gambia, yeye alisistiza ujumuishi katika matumizi ya intaneti Afrika.
"Mustakabali wa kidijitali wa afrika si kitu cha cha kununua kutoka nje— ni jambo tunalopaswa kuliunda kwa pamoja, kwa ujasiri, kwa maarifa na zaidi ya yote kwa imani thabiti. mtandao wa kidijitali uwe kwa manufaa ya wengi, si wachache; kwa maendeleo, na si kwa mgawanyiko", alisisitiza Mbow.
"Malengo yetu ya pamoja ni kujenga teknolojia"
Wadau wengine katika jukwaa hilo ni pamoja na mawaziri na wawakilishi wa serikali kutoka nchi za Afrika, ikiwamo Zambia, Afrika ya kusini, Nigeria, Togo, Kenya, Malawi na Namibia. Washiriki wengine katika jukwaa hilo ni wawakilishi wa umoja wa ulaya, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu,sayansi na utamaduni (UNESCO) na kampuni za kidijitali duniani.
Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, ametilia mkazo, kuhusu namna utawala na matumizi ya intaneti, kuimarisha taasisi, usalama wa kidijitali na kuendana na mabadiliko ya kasi ya intaneti duniani.
"Maendeleo ya kidijitali Afrika ni kipaumbele cha EU haliwezi kwisha , malengo yetu ya pamoja ni kujenga, na kuimarisha mapinduzi ya teknolojia."
Jukwaa hili la 14 la utawala wa intaneti Afrika lilianza jana ambapo wadau walijadili mistakabali wa intaneti, ujumuishi wa vijana na changamoto, fursa za akili mnemba.Leo Waziri mwenye dhamana ya teknolojia Jerry Silaa alifungua na Kesho jukwaa hilo litamalizia ngwe ya mwisho ya majadiliano.