Julia Greeley mtumwa wa zamani akaribia kupewa utakatifu
7 Juni 2018Wakati mtumwa huyo Julia Greeley ameshavuka viunzi muhimu ili awe mtakatifu, umetimia mwaka wa mia moja tangu aiage dunia. Picha ya pekee ya mama huyo inamwonyesha akiwa na msichana mdogo wa kizungu mikononi mwake. Alikuwa mtu wa tabaka la chini lakini kutokana na imani yake ya kidini ya upendo kwa binadamu wenzake, mtumwa huyo aliteka nyoyo za wengi wakati wa uhai wake.
Leo amekuwa mtumwa wa pekee aliyemo katika njia ya kupewa utakatifu. Kwa muda wa miaka mingi hata kabla ya kifo chake Julia Greeley alikuwa mtu maarufu katika mji wa Denver kwenye jimbo la Colorado. Watu walimwita mama huyo "malaika wa upendo wa binadamu."
Mtumwa huyo pia aliwasaidia masikini na mnamo mwaka 1880 alijiunga na Kanisa Katoliki ili kuwasaisia wale waliokuwa na dhiki kubwa zaidi.
Sio mengi yanayojulikana kuhusu mwanzo wa mama huyo mwema. Mtumwa huyo maarufu alizaliwa kati ya mwaka 1833 na 1848 na alipoteza jicho lake moja wakati msimamizi mmoja wa watumwa alipokuwa anamtandika viboko mama yake. Kwa bahati mbaya mjeledi wa ngozi aliokuwa anautumia msimamizi huyo wa watumwa ulimpiga usoni Julia Greeley.
Hata hivyo baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani vilivyopiganwa kuanzia mwaka 1861 hadi 1865 Julia Greeley alipata uhuru wake na alifanya kazi kama mutumishi wa nyumbani kwa matajiri weupe katika majimbo mbalimbali ya Marekani.
Hapo jana mabaki ya mama huyo yalizikwa tena kwenye kanisa kuu ya mjini Denver, miaka mia moja baada ya kufariki. Kasisi Jorge Rodriguez Novelo alimbariki mama huyo na alisema Julia Greeley ni mtu wa kwanza aliekuwa mtumwa kuzikwa hapo.
Wakati wa maisha yake Julia Greeley karibu muda wote alifanya kazi kwenye familia moja ya Wakatoliki. Mkuu wa familia hiyo baadae alipanda ngazi na kuwa gavana wa jimbo la Colorado na kutokana na mahusiano hayo, Julia aliweza kuchangisha fedha miongoni mwa matajiri kwa ajili ya kuwasiadia masikini. Kutokana na kuzijua hisia za watu weupe waliokuwa masikini ambao walipata misaada kutokana na fedha alizochangisha, Julia Greeley alifanya kazi ya kukusanya fedha nyakati za usiku ili majirani wasijue.
Mnamo mwaka wa 2016 mjadala juu ya kumfanya mama huyo kuwa mtakatifu ulianzishwa.
Idhini ya kufanyika misa ilitolewa na mabaki yake yamezikwa tena. Ripota mmoja wa gazeti la Denver Post, Frances Wayne amesema katika ripoti yake kwamba, Julia Greeley ni mwanamke aliyekuwa na moyo mkubwa wa upendo.
Mwandishi: Zaianab Aziz/KNA
Mhariri: Iddi Ssessanga