Jumuiya ya Cémac yakabiliwa na hatari ya mzozo wa kifedha
18 Desemba 2024Rais wa Cameroon Paul Biya amewaonya marais wenzake kwamba ikiwa hakuna kitakachofanyika, jumuiya ya Cémac itakabiliwa na matokeo mabaya, kwa nchi wanachama, lakini pia kwa ukanda huo wa Afrika ya Kati.
Kwa hiyo, kwa pamoja viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi na kifedha ya mataifa ya Afrika ya Kati wanatakiwa kukabiliana na mfumuko wa bei, kuzuia athari za madeni na mikopo inayozidi kiasi na kuzuia kushuka kwa thamani ya safaru yao ya pamoja ya Franc CFA.
Thierry Ndong, mwandishi wa habari wa masuala ya kiuchumi huko Yaoundé, amesema jumuiya ya Cemac inakaribia kutumbukia katika mzozo wa kifedha , licha ya bei ya mafuta kuwa nzuri kwa nchi wanachama ambao ni wazalishaji wa bidhaa hiyo.
"Tukizingatia ripoti ya Shirika la Fedha Ulimwenguni IMF, ile ya Benki ya Dunia na kwa kiasi fulani taarifa ya Benki Kuu ya Ufaransa ambako akaunti ya uendeshaji ya benki kuu ya nchi za Cémac inahifadhiwa ... ni kwamba hali ya kifedha ya Jumuiya hii ya kiuchumi ya Afrika ya Kati (Cémac) inatia wasiwasi. Karibu viashiria vyote vya kiuchumi viko kwenye taa nyekundu.", alisema Ndong.
Kulingana na ripoti ya 2024 ya Shirika la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa, UNDP ni kwamba Mataifa ya Jumuiya ya Cémac yanatatizika katika masuala ya maendeleo ya binadamu, licha ya rasilimali ghafi za ukanda huo. Ripoti hiyo inaonyesha viashiria dhaifu sana katika kupamabana na umasikini katika eneo hilo.
Tatizo la utawala bora Afrika
Ikiwa, viongozi wa kisiasa wakilinganisha hali hii mbaya ya kiuchumi na majanga ya hivi karibuni miaka, haswa mlipuko wa Covid-19 na mabadiliko ya tabia nchi, lakini wataalam wa kiuchumi wanatuhumu uongozi mbaya.
Djimadoum Mandekor, mtaalamu wa uchumi na fedha na afisa wa zamani wa Benki ya Mataifa ya Afrika ya Kati, anaamini kuwa utawala bora ndio msingi wa ukuaji wa uchumi jumuishi.
"Tafiti za shirika la IMF ambazo zilionyesha kuwa kama tungekuwa na kiwango sawa cha utawala kama wenzetu wa ECOWAS huko Afrika Magharibi, tungepata takriban asimilia mbili katika kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa. Kwa hivyo, unaona jinsi gani, suala la utawala bora ni muhimu kuhakikisha ukuaji ambao kila mtu anauita kuwa shirikishi, kwa manufaa ya zaidi ya Waafrika milioni 60 wa ukanda huu wa Afrika ya Kati.", alisisitiza Mandekor.
Umuhimu wa mageuzi ya kina
Wataalamu wa kifedha wametoa mwito kwa viongozi wa jumuiya ya kiuchumi na kifedha ya mataifa ya Afrika ya Kati kuzingatia mageuzi muhimu ilikufanikisha malengo ya jumuiya hiyo. Licha ya matumizi ya sarafu ya pamoja kwa nchi wanachama lakini bado jumuiya hii inajiburuta ukilinganisha na maeneo mengine ya Afrika kusini mwa jangwa la sahara.
Jumuiya ya Cémac inajumuisha nchi sita za Afrika ya Kati: Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo, Gabon, Guinea ya Ikweta na Chad.