1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ECOWAS kuendeleza vikwazo kwa wanachama waliofukuzwa

Zainab Aziz Mhariri:Saumu Njama
5 Juni 2022

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamesema vikwazo vitaendelea dhidi ya viongozi wa kijeshi wa Mali hadi pale watawala wa kijeshi watakapoharakisha mipango ya kurudisha madaraka kwa raia.

Nigeria | ECOWAS Gipfel
Picha: Präsidentschaft von Niger

Viongozi hao wamefikia uamuzi huo kwenye mkutano wa kilele wa nchi za kanda ya Afrika Magharibi uliofanyika siku ya Jumamosi. Viongozi hao walikutana kwenye mji mkuu wa Ghana, Accra kufanya maamuzi iwapo wataongeza vikwazo au wataziondolea vikwazo nchi ambazo zilikabiliwa na vikwazo na hatua nyingine za kinidhamu katika kanda hiyo.

​​Kiongozi wa serikali ya mpito ya Mali Kanali Assimi GoitaPicha: Annie Risemberg/AFP

Rais wa Tume ya ECOWAS Jean-Claude Kassim Brou amesema maifa15 wanachama wa jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS yamepanga kukutana tena tarehe 3 mwezi ujao wa Julai kubaini ikiwa nchi hizo tatu zilizosimamishwa uanachama wao za  Mali, Guinea na Burkina Faso zitawekewa vikwazo vingine zaidi au la.

ECOWAS tayari imeweka vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Mali mnamo mwezi wa Januari ambavyo vimetatiza biashara nyingi, pamoja na kufungwa kwa mipaka ardhini na angani kati ya Mali na nchi nyingine katika eneo hilo la Afrika Magharibi.

Luteni Kanali Paul-Henri Damiba, kiongozi wa kijeshi aliyempindua rais wa Burkina Faso mwezi Januari.Picha: Burkina Faso Presidency Press Service/REUTERS

Hatua hizo zimeudhoofisha mno uchumi wa Mali, na kusababisha wasiwasi juu ya kuzuka kwa mgogoro wa kibinadamu utakaoleta na madhara kwa raia wa Mali. 

Katika miezi iliyofuata baada ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS kuiwekea vikwazo Mali, kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita ameendelea kuchukua hatua nyingi ambazo nazo zinaendelea zaidi kuitenga Mali kimataifa, moja wapo ikiwa ni kuiondoa nchi yake katika kikosi cha usalama cha pamoja katika eneo la Afrika Magharibi na pia kuvifungia vyombo viwili vya habari vya Ufaransa kurusha matangazo nchini Mali.

Serikali ya Goita pia bado inasisitiza kuwa haitawezekana kufanyika uchaguzi nchini humo hadi ifikapo mwaka 2024 hatua ambayo inaongeza muda wake kubaki madarakani kwa karibu miaka minne licha ya hapo awali kukubaliana na kuwepo kwa serikali ya mpito kwa muda wa miezi 18 wakati ambapo Mali ilitarajiwa kufanya mabadiliko na kuelekea kwenye demokrasia.

Blaise Compaore aliyekuwa rais wa Burkina Faso kwenye mkutano na viongozi wa kijeshi wa Mali kabla ya kupinduliwa kwakePicha: Ahmed Ouoba/AFP/Getty Images

Viongozi wa kijeshi katika nchi za Guinea na Burkina Faso pia wamependekeza kuwepo serikali za mpito katika nchi hizo kwa muda wa miaka mitatu, mapendekezo ambayo yamekataliwa na jumuiya ya ECOWAS wamesema huo ni muda mrefu mno wa kusubiri hadi utakapofanyika uchaguzi mpya katika nchi hizo.

Viongozi wa mapinduzi ya kijeshi katika nchi zote tatu za Mali, Guinea na Burkina Faso wanaendelea kusisitiza kwamba itachukua miaka kadhaa kabla ya chaguzi kufanyika katika nchi zao.

Wimbi la mapinduzi ya kijeshi lilianza mnamo mwezi Agosti mwaka 2020, wakati Kanali Assimi Goita na wanajeshi wengine walipompindua rais wa Mali aliyechaguliwa kidemokrasia. Miezi tisa baadaye, walifanya mapinduzi ya pili na kumng'oa kiongozi wa mpito wa kiraia wa nchi hiyo ya Mali na kuchukua hatamu za urais yeye mwenyewe.

Rais wa Burkina Faso aliyepinduliwa Blaise Compaore Picha: Francois Mori/AP Photo/picture alliance

Msururu wa mapinduzi ya kijeshi katika nchi za Afrika magharibi umetokea wakati ambapo wadadisi wa kisiasa wengi walikuwa wanafikiri kwamba wanajeshi kunyakua madaraka ni jambo lililopitwa na wakati katika nchi hizo za Afrika Magharibi lakini kwa bahati mbaya hali sio kama walivyofikiria!

Kabla ya mapinduzi hayo ya kijeshi Mali ilikuwa imetulia kwa muda wa miaka minane na Guinea ilitulia kwa miaka kumi na tatu bila ya nchi hizo kushuhudia mapinduzi ya kijeshi.

Chanzo://AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW