1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

ECOWAS yaiondolea Niger baadhi ya vikwazo

Angela Mdungu
25 Februari 2024

Jumuiya ya ECOWAS imetangaza kuiondolea vikwazo vikali Niger, wakati ikitafuta mkakati mpya wa kuyazuia mataifa matatu yanayotawaliwa kijeshi kujiondoa kwenye Jumuiya hiyo ya kiuchumi.

Nigeria | Mkutano wa viongozi wa ECOWAS uliofanyika Abuja mwaka 2023
Wakuu wa Jumuiya ya ECOWASPicha: Kola Sulaimon/AFP

Kujiondoa kwa mataifa hayo katika jumuiya hiyo ya kiuchumi ni hatua inayotishia ushirikiano wa kikanda. Kauli ya ECOWAS imetolewa baada ya mkutano wa Jumamosi wa viongozi, uliojadili mzozo wa kisiasa ulioshamiri katika ukanda huo uliokumbwa na wimbi la mapinduzi ya kijeshi baada ya Niger, Burkina Faso na Mali kutangaza uamuzi wa kujionndoa kwenye jumuiya hiyo yenye nchi 15 wanachama.

Baada ya mkutano huo uliofanyika kwa faragha, ECOWAS ilisema kuwa imeamua kuondoa haraka vikwazo kwa Niger vikiwemo ufungaji wa mipaka, kuzishikilia mali za benki kuu na za nchi pamoja na kusimamishwa kwa miamala ya kibiashara.

Soma zaidi: ECOWAS yaangazia namna mpya ya kukabiliana na mizozo ya kikanda

Katika taarifa rasmi, Jumuiya hiyo imesema hayo yamefanyika kwa sababu za kiutu, lakini hatua hiyo inaonekana kama ishara ya kusawazisha hali wakati ECOWAS ikijaribu kuyashawishi mataifa hayo matatu kusalia kwenye muungano huo wa zaidi ya miaka 50.

Mpango wa kujiondoa wa Niger, Mali na Burkina Faso huenda ukasababisha mparaganyiko katika mtiririko wa huduma na biashara za Jumuiya hiyo zenye thamani ya karibu dola za kimarekani bilioni 150 kwa mwaka  

Zaidi taarifa iliyotolewa na jumuiya hiyo inazitaka nchi hizo zinazotawaliwa kijeshi kutathmini upya uamuzi wao kwa kuzingatia manufaa ambayo raia wa nchi wanachama wa ECOWAS  wanazozipata kupitia muungano huo. Imeongeza kuwa imeiondolea pia baadhi ya vikwazo Guinea inayotawaliwa licha ya kuwa taifa hilo halijasema linataka kujiondoa kwenye umoja huo.

Kufikiriwa upya kwa mkakati 

Awali, mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika ya Magharibi  ECOWAS Bola Tinubu alisema kundi hilo limefikia uamuzi wa kuufikiria upya mkakati wake, katika juhudi za kuzifanya nchi zirejeshe utawala unaofuata utaratibu wa kikatiba na amezitaka Niger, Burkina Faso, Mali na Guinea zisiichukulie Jumuiya hiyo kuwa adui.

Kiongozi wa kijeshi wa Niger Jenerali Abdourahamane TchianiPicha: ORTN/Télé Sahel/AFP/Getty Images

Vikwazo vimeilazimisha Niger ambayo tayari ni moja ya mataifa masikini zaidi duniani kupunguza matumizi ya serikali na kushindwa kulipa madeni yake ya zaidi ya dola za kimarekani milioni 500.

ECOWAS ilifunga mipaka yake na ikaiwekea vikwazo vikali Niger Julai 26 mwaka uliopita baada ya wanajeshi kumkamata Rais Mohamed Bazoum na kuanzisha serikali ya mpito.

Mapinduzi hayo ya kijeshi ya Niger ni mfululizo wa majeshi kutwaa madaraka hatua inayorudisha nyuma demokrasia katika Jumuiya hiyo. Katika taarifa yake, ECOWAS ilirudia kutoa wito wa kuachiliwa kwa Bazoum na kuwataka watawala wa kijeshi watoe ratiba inayokubalika ya kipindi cha mpito.

Hata hivyo Niger, Mali na Burkina Faso zimeuita mkakati huo kuwa ni kinyume cha sheria na zimesisitiza kujiondoa kwenye muungano huo bila ya kufuata taratibu za kawaida zinazopaswa kufuatwa ili kujitoa. Nchi hizo tatu tayari zimeanza kushirikiana chini ya muungano unaojulikana kama Muungano wa nchi za Sahel unaokusudia kuanzisha shirikisho .