1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya Kiislamu kukutana kuhusu mzozo wa Al Aqsa

24 Julai 2017

Jumuiya ya Mataifa ya Kiislamu OIC itakutana Istanbul kwa mazungumzo juu ya mzozo wa eneo linalozunguka msikiti wa Al-Aqsa.

Israel verschärfte Sicherheitsvorkehrungen am Tempelberg in Jerusalem
Picha: picture-alliance/newscom/D. Hill

Jumuiya ya Mataifa ya Kiislamu OIC itakutana mjini Istanbul kwa ajili ya mazungumzo juu ya mgogoro wa eneo linalozunguka msikiti wa Al-Aqsa wa mjini Jerusalem, baada ya mwishoni mwa wiki kutokea vurugu ambapo watu wanane wamefariki. 

Wakati huohuo mjumbe maalum wa Marekani anatarajiwa kuwasili nchini Israel leo hii katika jitihada za kupunguza mvutano uliotokana na hatua za kiusalama zilizochukuliwa na Israel.

Jumuiya ya Mataifa ya Kiislamu yenye wanachama 57 itafanya  mkutano wa ngazi ya mawaziri nchini Uturuki, ambayo sasa inashikilia urais wa OIC ili kujadili mvutano uliopo kati ya Israel na Palestina. 

Wakati huo huo Jordan imesema inajiandaa kumhoji afisa mmoja wa usalama wa Israel anayedaiwa kuwaua raia wawili wa Jordan katika ubalozi wa Israel mjini Amman lakini Israel inasema kuwa afisa huyo ana kinga ya kidiplomasia hivyo basi bado pendekezo la Jordan linashughulikiwa.

Mohammed Jawawdeh aliyekuwa na umri wa miaka 17 alikufa papo hapo na wa pili alikuwa daktari Baashar Hamarneh aliyekuwepo katika ubalozi huo na ambaye alifariki baadaye akiwa hospitalini. Mkurugenzi mwandamizi wa usalama katika ubalozi wa Israel nchini Jordan alipata majeraha baada ya kushambuliwa na Jawawdeh na anaendelea kupata matibabu hospitalini.

Mjumbe maalum wa Marekani Jason Greenblatt nchini IsraelPicha: picture alliance/AP Photo/E. Agostini

Vilevile ziara ya mjumbe maalum wa Marekani Jason Greenblatt nchini Israel inafanyika baada ya kipindi cha zaidi ya wiki moja ya mvutano juu ya eneo linalojumuisha msikiti wa Haram al-Sharif unaojulikana na Wayahudi kama Temple Mount ambao ndiyo kitovu cha mzozo kati ya Israeli na Palestina.

Mjumbe huyo maalum anatarajiwa kuwasili nchini Israel leo hii katika jitihada za kupunguza mvutano uliotokana na hatua mpya za kiusalama zilizochukuliwa na Israel baada ya kutokea vurugu za mwishoni mwa wiki ambazo zilisababisha vifo vya watu wanane.

Israel imeweka vifaa vya ukaguzi wa kielektoniki katika eneo takatifu la msikiti wa Al Aqsa baada ya mashambulio yaliyotokea mnamo tarehe 14 ambapo polisi wawili wa Israel waliiuwawa. 

Maafisa wa usalama wa Israel wanasema vifaa hivyo ni muhimu na kama vingelikuwepo mapema washambuliaji wasingeliweza kuingiza bunduki katika eneo hilo. Wapalestina wanaiangalai hatua hiyo ya kuimarisha ulinzi kama njia ya Israel ya kutaka kuwa na udhibiti zaidi wa eneo hilo.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/APE

Mhariri: Saumu Yusuf