1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya Kimataifa yaichangia Sudan dola bilioni 1.8

Admin.WagnerD26 Juni 2020

Mataifa ya magharibi na yale ya kiarabu yameahidi mchango wa dola bilioni 1.8 kuisaidia Sudan inayoandamwa na hali mbaya uchumi, tangu vuguvugu la demokrasia lilipoung´oa utawala wa muda mrefu wa rais Omar al-Bashir.

Sudan Premierminister Abdalla Hamdok
Waziri Mkuu wa Sudan Abdalla HamdokPicha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Ahadi hiyo kutoka zaidi ya mataifa 40 ikiwemo msaada wa nyongeza wa dola milioni 400 kutoka benki ya dunia, imetolewa wakati wa mkutano uliotishwa na Ujerumani kwa lengo la kuisaidia serikali ya mpito nchini Sudan baada ya miongo kadhaa ya vikwazo vya kiuchumi na kutengwa kimataifa chini ya utawala wa al-Bashir.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas aliuambia mkutano huo uliofanyika kwa njia ya video kuwa msaada uliotolewa ni hatua ya kwanza ya kuisaidia Sudan na kwamba kutakuwa na mkutano mwingine wa wafadhili mapema mwaka unaokuja.

Akitoa ahadi ya mchango wa Ujerumani kwa Sudan waziri wa ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo wa serikali ya shrikisho Gerd Muller amesema:

"Tayari kwa sehemu tumechukua hatua kwenye maeneo ya kipaumble ya ajira na mafunzo ya ufundi, usalama wa chakula na utowaji wa huduma za msingi. Tutaendelea kutanua ushirkiano huu zaidi, pamoja na mwenzangu Heiko Maas ninaahidi kwa niaba ya serikali ya Ujerumani msaada jumla wa euro milioni 150 kwa Sudan kwa mwaka 2020"

Guterres na Hamdok wasifu juhudi ya kuisaidia Sudan

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: webtv.un.org

Akizungumza wakati wa mkutano huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msaada wa kifedha kwa taifa hilo linajikongoja ili kuenzi mageuzi ya kidemokrasia yaliyopatikana pamoja na kuhakikisha utulivu nchini Sudan.

Waziri mkuu wa Sudan Abdalla Hamdok ameshukuru na kusifu jitihada hiyo ya kuipiga jeki nchi yake ambayo inapitia kipindi kigumu cha mpito chini ya serikali ya mseto kati ya raia na majenerali wa jeshi.

Mataifa yaliyoichangia fedha nchi hiyo ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Muungano wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia pamoja na taasisi za kikanda ikiwemo Umoja wa Ulaya na mashirika ya fdha ya kimataifa.

Fedha zilizotolewa bado ni kidogo 

Picha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Hata hivyo kiwango kilichotolewa na mkutano huo ni kidogo ikilinganishwa na ombi la dola bilioni 8 lililotolewa na serikali ya Sudan ili kunusuru uchumi wa taifa hilo unaoandamwa na ukosefu wa ajira na athari za janga la virusi vya corona.

Sehemu kubwa ya fedha zilizoahidiwa wakati wa mkutano wa jana zitatumika kufadhili mpango wa aina yake wa dola bilioni 1.9 wa kuzipatia familia masikini fedha za kujikimu katika kipindi cha miaka miwili inayokuja.

Upungufu wa mahitaji muhimu umezusha mfadhaiko nchini Sudan na kuwalazimisha maelfu ya raia wake kupanga foleni kwa saa kadhaa kunua mkate au mafuta.

Theluthi mbili ya raia milioni 40 wa taifa hilo wanaishi katika umasikini na serikali ya mpito imerithi deni la dola bilioni 60 na mfumuko mkubwa wa bei.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW