Jumuiya ya kimataifa yaisaidia Afghanistan
6 Oktoba 2016Hata hivyo kiwango hicho hakijafikia lengo la mpango wake wa kuanza upya mkakati wa kuisaidia nchi hiyo.
Afghanistan inasalia kuwa mmoja ya nchi masikini zaidi na isiyo na uthabiti wa kisiasa ikilinganishwa na nchi ningine duniani, pamoja na misaada ya mabilioni ya fedha katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Rushwa ni tatizo kubwa, wakati ambapo suala la usalama linasalia kuwa na mashiko makubwa baada ya Jumuiya ya kujihami ya Umoja wa Ulaya, NATO kukamilisha mpango wake wa kukabiliana na ugaidi mnamo mwaka 2014.
Lengo la mkutano huo ulioandaliwa na Umoja wa Ulaya lilikuwa ni kuendelea kuisaidia Afghanistan kwa miaka minne ijayo, kwa kiwango cha Dola Bilioni 4 kwa kila mwaka, zilizoahidiwa mwaka 2012.
Pamoja na kwamba msaada huo haukufikia lengo halisi, ahadi zilizofikiwa Jumatano hii kwenye mazungumzo hayo, ahadi zilizotolewa zilizidi matarajio, amesema mwakilishi wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini.
Msaada huo, ambao unazingatia zaidi katika kuisaidia Afghanistan kurejea katika utangamano wa kisiasa, utalenga pia kufanya maboresho mapya ya serikali ya afghanistan, ambayo ni pamoja na kuimarisha demokrasia na kupambana na rushwa. Umoja wa Ulaya na mataifa wanachama wameahidi kiasi cha Dola Bilioni 5.6 kwa kipindi cha miaka minne ijayo, amesema Mogherini. Kiasi hiki ni cha kiwango cha juu katika fedha za msaada zilizotolewa kwenye nchi hiyo, amesema Rais wa baraza la Umoja wa Ulaya, Donald Tusk.
Wakati hatua hiyo inafikiwa, mapigano makali katika mji wa Kunduz ulioko eneo la Kaskazini mwa Afghanistan, yamesababisha watoa huduma za afya kukimbia mji huo ili kulinda usalama wao. Taarifa ya maafisa iliyotolewa Alhamisi hii imeeleza kuwa hatua hiyo imesababisha kukosekana kabisa kwa huduma hizo za afya. Hali ya kibinaadamu imeendelea kuathirika na kuwa mbaya zaidi wakati mapigano hayo kati ya wapiganaji wa Taliban na majeshi ya usalama ya Afghanistan, yanapoingia katika siku yake ya nne.
Majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na vikosi maalumu vya serikali ya Marekani na vile vinavyoshambulia toka angani, yamerejelea kauli yake kwamba wanaushikilia mji huo wa Kunduz, wakati taarifa kutoka kwa wakazi wa eneo hilo zinasema mapigano hayo makali yamesababisha raia wengi kuukimbia mji huo.
Serikali ya Afghanistan imesema majeshi ya usalama yamefanikiwa kuyachukua maeneo mengi ya Kunduz kutoka kwa wapiganaji wa Taliban na hivi sasa wanapambana na wapiganaji hao kwenye eneo lililoko nje ya viunga vya mji, kama anavyoeleza mmoja wa askari wa vikosi vya uslama vya Afghanistan Ali Reza.
Shambulizi kwenye mji wa Kunduz lilianza usiku wa Jumapili hii, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Taliban kuuchukua mji muhimu wa kimkakati kwa takriba wiki mbili, mnamo mwezi Septemba mwaka 2015, hatua iliyoleta mshituko kwa serikali ya Afghanistan pamoja na Jumuiya ya kimataifa.
Mwandishi: Lilian Mtono/Dpa/Rtre/Ap
Mhariri: Idd Ssessanga.