Jumuiya ya kimataifa yakemea mpango wa nyuklia wa Putin
27 Machi 2023Rais wa Urusi Vladimir Putin alitangaza siku ya Jumamosi kuwa, nchi yake itaweka silaha za kivita za nyuklia huko Belarus hatua alioitaja kuwa ni sawa na Marekani ilivyohifadhi silaha kama hizo katika mataifa kama Ujerumani,Ubelgiji na Uturuki.
Ingawa tangazo hilo haikutarajiwa ni moja ya ishara za nyuklia zinazotolewa na Urusi na onyo kwa jumuiya ya kujihami ya NATO dhidi ya uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Ukraine, iliotaka kuitishwa kwa mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kujibu hatua hiyo ya Urusi.
Soma pia:NATO yaapa kuiunga mkono Ukraine bila kuchoka
NATO kupitia msemaji wake Oana Lungescu amesema katika taarifa yake kwamba Urusi mara kwa mara imekuwa ikivunja ahadi zake kuhusu udhibiti wa silaha zake za kimkakati za nyuklia na kuongeza kwamba jumuiya hiyo ipo inafuatilia kwa ukaribu hatua za Urusi.
Tangazo hilo la Urusi pia limekosolewa vikali na Ukraine kupitia mkuu wake wa usalama Oleksiy Danilov akisema, mpango wa Urusi utaivuruga Belarus ambayo aliitaja kushikiliwa kama "mateka wa nyuklia" na Moscow.
Lithuania nayo imeweka bayana kutoa vikwazo vipya kwa Moscow na Minsk endapo mpango huo utatekelezwa.
EU:Tutajibu kwa vikwazo zaidi ikiwa Belarus itatekeleza mpango
Tangazo hilo la Urusi lililoongeza hofu juu ya vita vya nyuklia kwa mujibu wa wataalamu, pia limelaani vikali na Umoja wa Ulaya ulioitaka Belarus kutoshiriki mpango huo.
Mkuu wa sera za kigeni Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema Belarus kukaribisha silaha za nyuklia za Urusi kunaweza kumaanisha kuongezeka kwa kutowajibika na tishio kwa usalama wa Ulaya na kwamba Umoja huo upo tayari kujibu kwa vikwazo zaidi.
Hata hivyo Marekani ambayo nayo ni miongoni mwa mataifa yanayomiliki silaha za kimkakati za nyuklia imepuuza juu ya mpango wa Urusi kupeleka silaha hizo Belarus.
Soma pia:Umoja wa Ulaya kusaidia kuandaa mkutano wa kuwarejesha watoto wa Ukraine
Msemaji wa Ikulu ya Marekani Johnn Kirby alisema hawajaona dalili zozote kwa rais Vladimir Putin kujiandaa katika kutumia silaha hizo.
"Pia naweza kukuambia kuwa hatujaona chochote ambacho kingetufanya kubadili mkakati wetu wa kuzuia nyuklia."Alisema Kirby
Belarus na Urusi zina uhusiano wa karibu kijeshi, na Minsk iliruhusu Moscow kutumia eneo la Belarus kama kituo cha uvamizi wake kamili wa Ukraine mwaka jana.
Mji wa Avdiivka washambuliwa na vikosi vya Urusi
katika uwanja wa mapambano huko Ukrainemakombora ya Urusi yamesababisha kufungwa kabisa kwa mji wa Avdiivka uliopo kusini magharibi mwa Bakhmut.
Jeshi la Ukraine wiki iliopita lilionya juu ya mapigano makali katika mji wa Avdiivka huku likisema kuwa katika saa 24 vikosi vya kyiv vimezuia mashambulio 85 ya Urusi katika eneo la Mashariki ikiwemo Bakhamut.
soma pia:Vikosi vya Urusi vyabadili mwelekeo wake Bakhmut
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema Jumapili kwamba vikosi vyake vilishambulia maeneo ya kijeshi katika mikoa ya Kharkiv, Donetsk, Zaporizhzhia na Kherson, na kusababisha hasara kubwa ya Ukraine.