Jumuiya ya kimataifa yalaani shambulizi Somalia
4 Desemba 2009Wakati huo huo msemaji wa kundi kubwa la waasi nchini Somalia la al Shabaab amekana leo kuwa kundi hilo linahusika na shambulio hilo.
p>Rais wa halmashauri ya umoja wa Afrika Jean Ping ameshutumu vikali shambulio hilo lililotokea jana .Kitendo hicho cha kinyama ambacho kinalenga katika kuharibu utaratibu wa kuleta amani hakitazuwia umoja wa Afrika kutoa msaada kwa serikali ya mpito ya Somalia kuleta hali ya maridhiano nchini humo, imesema taarifa iliyotolewa na ofisi ya rais wa halmashauri hiyo .
Wakati huo huo katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki-moon na baraza la usalama la umoja wa mataifa limeshutumu vikali shambulio hilo.
Katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa shambulio hilo litaimarisha tu nia ya serikali ya Somalia na watu pamoja na washirika wengine kuendelea na juhudi zao za kupambana na ugaidi nchini Somalia.
Hili amesema katibu mkuu Ban Ki-moon kuwa ni shambulio la kihalifu dhidi ya watu ambao wana nia ya kuleta maendeleo kwa njia ya amani.
Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na umoja wa mataifa ya rais Sheikh Sharif Ahmed inadhibiti mitaa michache tu ya mji mkuu Mogadishu.
Siku chache kabla ya shambulio la jana , wakaazi wamesema kuwa serikali ilikuwa inapanga shambulio jipya dhidi ya waasi.
Mkaazi mmoja wa mjini Mogadishu Badra Yussuf Ali hata hivyo amesema kuwa jamii imeingiwa na hofu kubwa kutokana na shambulio hilo la kujitoa muhanga.
Hali kwa sasa iko shwari na hata hoteli palipotokea shambulio hilo ni shwari. Watu bado wana majonzi baada ya shambulio hilo na kuna hali ya taharuki katika jamii.
Waziri wa afya wa Somalia Qamar Aden Ali, waziri wa elimu Ahmed Abdulahi Waayeel na waziri wa elimu wa juu Ibrahim Hassan Addow waliuawa katika shambulio hilo.
Waziri wa michezo Saleban Olad Roble amejeruhiwa na yuko katika hali mbaya.
Wakati huo huo msemaji wa kundi la wapiganaji wa al- Shabaab amekana leo kuwa kundi hilo limehusika katika shambulio hilo la hapo jana.
Wanafunzi pamoja na wazazi wao ni miongoni mwa watu waliouwawa katika shambulio hilo.
Msemaji wa Al-Shabaab Sheikh Ali Mohammed Rage amewaambia waandishi habari kuwa kundi hilo halikuhusika na shambulio hilo.
Amesema kuwa kundi hilo linaamini kuwa huenda na njama iliyofanywa na serikali yenyewe.
Ameongeza Rage kuwa hiyo si katika utaratibu wa kundi la al Shabaab kushambulia watu wasio na hatia. Rage amesema kuwa mgawanyiko mkubwa wa kisiasa umejitokeza kati ya viongozi wa juu wa serikali katika serikali ya rais Sheikh Sharif Ahmed mjini Mogadishu. Amedokeza kuwa tunafahamu baadhi ya maafisa wa serikali waliondoka katika eneo hilo dakika chache kabla ya shambulio. Na hii inaonyesha kuwa wanahusika na shambulio hilo.
Mwandishi:Sekione Kitojo
Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman