Jumuiya ya Madola yaahirisha mkutano kutokana na corona
22 Aprili 2020Taarifa ya sekretarieti ya jumuiya hiyo yenye makao yake makuu mjini London, Uingereza imesema kuwa tarehe mpya ya mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka miwili, itatangazwa kwa wakati unaofaa.
Jumuiya ya Madola ambayo inaundwa na nchi 54 zilizotawaliwa na Uingereza na watu bilioni 2.4, mwezi uliopita ilisema kwamba inaitathmini hali inavyoendelea tangu virusi vya corona vilipozuka.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Patricia Scotland anasema janga la virusi vya corona limebadilisha mwenendo wa historia yao ya sasa, wakati ambapo serikali ulimwenguni kote zikiwa zinapambana kuzuia maambukizi yasienee.
Maamuzi ya kihistoria
"Lazima tuwe waangalifu kuhusu hatari inayoweza kusababishwa na mikutano mikubwa. Mazingira yaliyopo sasa yanahitaji maamuzi ya kihistoria," alifafanua Patricia, huku akiahidi kutoa msaada kamili kwa nchi zote zilizoathirika.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema: "Tunatarajia kuikaribisha familia ya Jumuiya ya Madola mjini Kigali kwa ajili ya mkutano wa wakuu wa serikali za Jumuiya ya Madola, CHOGM pindi janga hili litakapotokomezwa kabisa."
Serikali ya Kagame ilikuwa ni moja kati ya nchi za kwanza barani Afrika kutangaza kusitisha kabisa shughuli za kijamii kwa lengo la kujaribu kuzuia kuenea kwa COVID-19.
Wanasiasa na wafanyakazi wa ngazi ya juu serikalini pia walielekeza sehemu ya mishahara yao ipelekwe kuwasaidia watu walioathirika kiuchumi kutokana na kufungwa kwa shughuli hizo nchini Rwanda.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Habari la Ufaransa, AFP, bara la Afrika lina visa 23,251 vya COVID-19 ambavyo vimethibitishwa na watu 1,161 wamekufa. Rwanda ina wagonjwa 147 wa virusi vya corona, lakini haijarekodi kifo chochote.
(AFP)