1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Stoltenberg apuuza vitisho vya Urusi, aomba Ukraine ilindwe

31 Mei 2024

Katibu Mkuu wa mfungamano wa kijeshi wa NATO, Jens Stoltenberg amepuuza vitisho vilivyotolewa na Urusi juu ya kukolea zaidi kwa vita vya Ukraine.

Miaka 75 ya NATO I NATO - Jens Stoltenberg
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kijeshi NATO Jens Stoltenberg apuuza maonyo ya Urusi baada ya Marekani kutaka Ukraine kutumia silaha zake ndani ya UrusiPicha: Michal Kamaryt/CTK/picture alliance

Stoltenberg ameashiria hatua hiyo baada ya Marekani kuruhusu silaha zake zitumiwe na majeshi ya Ukraine kushambulia ndani ya Urusi.

Akizungumza kando ya mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa NATO mjini Prague, Stoltenberg amesema Jumuiya ya NATO imesikia mara nyingi maonyo ya aina hiyo kutoka Urusi akisisitiza kwamba kuisaidia Ukraine kujilinda hakumaanishi kwamba nchi washirika wa Ukraine wanachochea vita zaidi.

Katibu Mkuu wa NATO Stoltenberg amewaambia waandishi wa habari mjini Prague kuwa anaunga mkono msaada unaotolewa na washirika kwa Ukraine na amezitaka nchi wanachama wa NATO kuongeza misaada ya kijeshi ya kila mwaka kwa Ukraine hadi euro bilioni 40 kama kima cha chini.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za NATO wanakutana kwenye mji huo mkuu wa Jamhuri ya Czeck kujadili usalama barani Ulaya na suala hilo la msaada wa muda mrefu kwa Ukraine.