1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya Nchi za Kiarabu: Lazima Assad aondoke

23 Julai 2012

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Jumuiya ya nchi za kiarabu wamemtolea wito rais Bashar al-Assad kuachia madaraka ili kuepusha umwagaji zaidi wa damu, na kumuahidi njia salama ya kuondokea iwapo atafanya hivyo.

Shinikizo lashamiri kwa Bashaar al-Assad aondoke
Shinikizo lashamiri kwa Bashaar al-Assad aondokePicha: Reuters

Wito wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kumtaka rais Bashar al-Assad aachie madaraka umetolewa katika tangazo la pamoja baada ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi za Jumuiya ya mataifa ya Kiarabu ambayo yamemalizika usiku wa manane katika mji mkuu wa Quatar, Doha. Maazimio ya mkutano huo yametangazwa na Waziri Mkuu wa Qatar Sheikh Hamad bin Jassim al-Thani.

''Tumemtaka Bashar al- Assad kuachia madaraka, na tumeahidi kumpa njia salama ya kuondokea. Vile vile tumeahidi mchango wa fedha, kiasi cha dola milioni 100 kuwasaidia wakimbizi wa Syria, hali kadhalika tumezungumzia majukumu ya mpatanishi Kofi Annan, ambayo sasa yanapaswa kujikita kwenye matayarisho ya kuundwa kwa kipindi cha mpito''. Amesema Sheikh Hamad.

Waasi watakiwa kuunda serikali

Riad al Asaad, kamanda wa Jeshi Huru la SyriaPicha: dapd

Mkutano huo umekitaka kikundi cha waasi kijulikanacho kama Jeshi Huru la Syria kuunda kushirikiana na kile kilichotajwa kuwa ''uongozi halisi wa taifa'', kuunda serikali ya mpito. Hakukuwa na maelezo zaidi juu uongozi huo uliotajwa. Nchi za kiarabu zimetaka uitishwe mkutano wa dharura wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuamua juu ya kutengwa kwa eneo salama na njia ya kupitishia msaada wa kibinadamu nchini Syria.

Jana Marekani ilisema itamwajibisha afisa yeyote wa Syria ambaye atahusika katika kutumia silaha za kikemikali za nchi hiyo. Onyo hilo limetolewa baada ya kuenea kwa ripoti kwamba rais Bashar al-Assad alikuwa tayari kutumia silaha hizo ili kuunusuru utawala wake unaosakamwa.

Jeshi larudisha wilaya mbili za Damascus

Mji mkuu wa Syria Damascus umegeuka uwanja wa mapambanoPicha: dapd

Nchini Syria kwenyewe, kikosi cha jeshi la serikali chenye kuongozwa na kaka mdogo wa rais Assad kimewashambulia waasi mjini Damascus kwa kutumia helikopta. Mapigano pia yameripotiwa katika mji wa Aleppo, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Syria. Shirika la habari la Serikali, SANA limesema jeshi limekisafisha kitongoji cha Qamoon na kuwafurusha wale lililowaita magaidi.

Televisheni ya taifa imeonyesha picha za maiti, silaha na vyombo vya mawasiliano ambavyo imesema vimetekwa kutoka kwa waasi. Imesema baadhi ya wapiganaji waliouawa walikuwa na vitambulisho vya Jordan na Misri, na kuzishutumu nchi za kigeni kuwapa mafunzo waasi na kuwatuma nchini Syria. Hata hivyo kituo hicho cha serikali kimekanusha ripoti kwamba helikopta zimetumiwa katika operesheni hizo.

Ongezeko la vifo na wakimbizi

Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema kuwa kikosi cha kaka wa rais Assad kimeuvamia mtaa wa Barzeh likitumia vifaru na magari ya kivita, huku walenga shabaha wakiwa wamewekwa kwenye mapaa ya nyumba.

Shirika hilo limesema kuwa watu 123 waliuawa jana nchini Syria, 59 kati yao wakiwa raia, na kuongeza kuwa idadi ya waliokufa tangu kuanza kwa uasi nchini Syria miezi 16 iliyopita imefikia watu 19,000.

Jeshi la serikali na waasi pia wamekabiliana katika maeneo ya mpaka kati ya Syria na nchi za Jordan, Irak na Uturuki kuwania udhibiti wa vituo vya mpakani. Ghasia hizi zimesababisha idadi kubwa ya wakimbizi kukimbilia Lebanon, Jordan na Uturuki.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP/RTRE/DPA

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi