Jumuiya ya SADC kusimamisha uanachama wa Madagascar
30 Machi 2009Viongozi wa jumuiya ya kiuchumi ya kanda ya kusini mwa Afrika, SADC, wanatarajiwa hii leo kusimamisha uanachama wa Madagascar katika jumuiya hiyo baada ya rais wa nchi hiyo kuondolewa madarakani mapema mwezi huu. Kwenye mkutano wake unaofanyika mjini Mbambane nchini Swaziland, jumuiya ya SADC pia inadurusu mpango wa kuufufua uchumi wa Zimbabwe.
Viongozi wa serikali za nchi wanachama wa jumuiya ya SADC hii leo wamelaani vikali hatua ya kumng´oa madarakani rais wa Madagascar Marc Ravalomanana, hatua iliyoungwa mkono na jeshi la nchi hiyo. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa SADC mjini Mbambane nchini Swaziland, Mfalme Mswati III wa nchi hiyo, amesema hatua ya Andry Rajoelina kunyakua madaraka nchini Madagascar inakiuka misingi, itifaki na mikataba na ni hatua isiyokubalika. Aidha mfalme Mswati III amesema na hapa namnukulu, "Tuko hapa kujadiliana njia muafaka ya kushughulikia hali nchini Madagascar," mwisho wa kmunukulu mfalme huyo.
Rais wa zamani wa nchi hiyo, Marc Ravalomanana, aliyejiuzulu kufuatia shinikizo kutoka kwa jeshi wakati lilipomuunga mkono mpinzani wake, Andry Rajoelina, amewasili saa moja baada ya mkutano kuanza na kuwahutubia viongozi wa SADC kuhusu hali nchini mwake. Viongozi wa SADC wanatakiwa kuamua kuhusu njia ya kukabiliana na hali ya kisiasa nchini Madagascar.
Timu ya usalama inayoongozwa na mfalme Mswati III tayari imeonya kwamba jumuiya ya SADC huenda ikaiwekea vikwazo serikali ya rais Rajoelina na imetuma tume ya uchunguzi nchini Madagascar. Mkurugenzi mtendaji wa SADC, Tomaz Salomao, aliiongoza tume hiyo na alitarajiwa kuongoza mijadala kuhusu njia za kuisaidia Madagascar kurejea katika demokrasia.
Siku ya Jumapili wajumbe kwenye kikao cha mawaziri wa kigeni wa nchi za SADC, ambao wanatakiwa kutoa pendekezo kwa mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo, walipendekeza kuwa Madagascar huenda isimamishwe kuwa mwanachama wa SADC na kusisitiza uchaguzi wa mapema ufanyike. Msimamo huo wa SADC huenda ukamtenga rais Rajoelina aliyenyakua madaraka katika hatua iliyoelezwa kuwa mapinduzi na jumuiya ya kimataifa.
Umoja wa Afrika uliusitisha uanachama wa Madagascar katika umoja huo Machi 20 mwaka huu, na kuupa utawala wa nchi hiyo miezi sita kuitisha uchaguzi kwa mujibu wa katiba. Rais Rajoelina ameweka kipindi cha miaka miwili cha utawala wa mpito.
Mkutano wa jumuiya ya SADC mjini Mbambane Swaziland pia unajadili juhudi za kuunga mkono mpango wa kuufufua uchumi wa Zimbabwe. Mgogoro wa kiuchumi unaoiathiri Zimbabwe umesababisha ukosefu wa ajira kufikia asilimia 90 nchini humo. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Afrika Kusini, Nkosazana Dlamini-Zuma amesema leo kwenye mkutano wa SADC kwamba Zimbabwe imeomba dola kati ya bilioni 8 na 10 za kiamrekani kama msaada wa kusaidia juhudi za kuufufua uchumi wake.
Dlamini-Zuma amesema jumuiya ya SADC inadurusu mpango wa Zimbabwe unaohitaji kitita hicho cha fedha. Kiwango hicho ni karibu mara mbili ya kile ambacho waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai, alisema kilihitajika kuufufua uchumi wa nchi hiyo.