Juncker aeleza matumaini baada ya Brexit
13 Septemba 2017Katika hotuba yake ya hali ya Umoja wa Ulaya, Juncker amesema kundi hilo la mataifa limekuwa na umoja zaidi kufuatia mlolongo wa mizozo, na kusisitiza kasi ya kiuchumi inaanza kuonekana.
Waziri mkuu huyo wa zamani wa Luxembourg ameuhimiza Umoja wa Ulaya kuimarisha hatua ya mataifa hayo kuwa pamoja zaidi, na pia alisema Umoja huo unapaswa kujaribu kufikia makubaliano ya kibiashara na Australia na New Zealand ifikapo mwishoni mwa muhula wake madarakani.
Juncker alionesha matumaini zaidi katika hali bora ya kiuchumi katika mataifa hayo kuliko ilivyokuwa wakati alipohutubia bunge hilo la Ulaya mjini Strassbourg Septemba 2016 , akikiri wakati huo kwamba , "ni wazi kwa kila mtu kuona kwamba Umoja wetu hauko katika hali nzuri, ukivurugwa na mwaka ambao ulitikisa msingi wa Umoja huo.
Lakini wakati kuibuka kwa siasa kali za mrengo wa kulia , baada ya Brexit na kuchaguliwa kwa rais Donald Trump nchini Marekani , kukionekana kudhibitiwa hivi sasa, Juncker amesema viongozi wa mataifa 27 yaliyobakia katika Umoja wa Ulaya wamejiunga pamoja nyuma ya miito yake ya Umoja.
Wito wake wa kuongeza ushirikiano hata hivyo ulienda sambamba na haja ya kuponesha mgawanyiko mkubwa na mataifa ya ulaya mashariki ambayo yanazuwia hatua yoyote zaidi ya ujumuisho katika Umoja huo. Juncker alisema:
"Sasa ni wakati wa kujenga Ulaya iliyo na Umoja zaidi, imara na yenye demokrasia zaidi kwa ajili ya mwaka 2025."
Waziri wa fedha wa EU
Juncker mwenye umri wa miaka 62 , ana chini ya miaka miwili kubaki madarakani akiwa mkuu wa chombo hicho chenye nguvu cha utendaji cha Umoja wa Ulaya kuhakikisha kwamba atakayoyaacha sio tu kujitoa kwa mwanachama mkubwa katika Umoja huo.
Juncker amesema kuna haja kwa Ulaya kuwa na waziri maalum wa fedha, ikiwa hatua kubwa kuelekea kanda ya euro kujumuika zaidi.
Juncker pia amezungumzia kuhusu Uturuki akisema nchi hiyo inajitenga kutoka Ulaya na haitakuwa mwanachama wa kundi hilo la mataifa katika kipindi cha karibuni.
Kuhusu wakimbizi na wahamiaji, rais huyo wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya amesema , Ulaya inapaswa kuchukua jukumu la pamoja kusaidia kuweka mazingira kuwa bora zaidi katika vituo vya kuwahifadhi wahamiaji nchini Libya. Juncker amewaambia wabunge wa Ulaya kwamba Umoja huo unapaswa kufanyakazi kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la kuwajhudumia wakimbizi kuhakikisha kwamba hali hiyo ya kudhalilisha haiendelei.
Pia amesema ataomba kupewa madaraka kuchunguza wawekezaji wa nje wanaotaka kununua sekta muhimu za kimkakati barani Ulaya, huku kukiwa na wasi swasi juu ya uwekezaji wa China barani humo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / dpae /
Mhariri: Iddi Ssessanga