1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juncker atoa hotuba yake ya mwaka katika bunge la Ulaya

12 Septemba 2018

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, katika hotuba yake ya kila mwaka katika bunge la Ulaya ametoa mwito wa kuanzishwa kwa ushirikiano mpya na bara la Afrika.

Europäisches Parlament in Straßburg | Rede zur Lage der EU von Jean-Claude Juncker
Picha: Reuters/V. Kessler

Wito wa mkuu huyo wa tume ya Ulaya wa kuanzishwa kwa ushirikiano mpya na bara la Afrika umetolewa wakati ambapo nchi za Ulaya zinajitahidi ili kupata suluhisho la pamoja kwa ajili ya kupunguza kasi ya mtiririko wa wahamiaji kutoka Afrika wanaotaka kuingia Ulaya huku wakihatarisha maisha yao kwa kuivuka bahari ya Mediterania. Wahamiaji hao hasa huingia katika nchi za Uhispania na Italia, na lengo lao kubwa huwa ni kutafuta maisha bora.

Bwana Juncker amesema inapasa kuwa na makubaliano mengi ya biashara kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya yenye lengo la kuzinmgatia biashara huru baina ya  bara na bara jingine.

Rais wa tume ya Ulaya Jean Claude Juncker amesema ushirikiano mpya wa kiuchumi kati ya mabara haya mawili unatarajiwa kuunda nafasi za ajira hadi milioni 10 huko Afrika katika kipindi cha miaka mitano tu. Amesisitiza kuwa mahusiano ya Umoja wa Ulaya  na Afrika hayapaswi kupewa mtazamo wa misaada ya maendeleo pekee.

Wajumbe wakimsikiliza rais wa tume ya Ulaya Jean Claude Juncker alipotoa hotuba yake ya mwaka kwenye bunge la Umoja wa Ulaya mjini StrasbourgPicha: Reuters/V. Kessler

Ujumbe huo wa mkuu wa tume ya Ulaya unailenga miji mikuu katika bara la Afrika ambapo serikali za Ulaya zina hamu kubwa ya kuongeza ushirikiano wake katika kuwahamasisha wahamiaji kubakia  nyumbani. Rais wa tume ya Ulaya Jean-Claude Juncker ametaka pia juhudi zifanyike kwa ajili ya kuimarisha sarafu ya Euro ili iweze kushindana na Dola na kufikia katika kiwango cha sarafu za kimataifa.

Juncker alimeiambia bunge la Ulaya mjini Strasbourg wakati alipowasilisha mpango wake wa kila mwaka amesema kuwa ni ajabu kwamba makampuni ya Ulaya yanunua ndege za Ulaya kwa kutumia dola ya Marekani badala ya euro. Amehimiza kwamba sarafu ya euro lazima iwe uso wa Ulaya mpya iliyo huru. Juncker amezitaka nchi za Ulaya ziwe katika mstari wa mbele kwenye  masuala ya kimataifa na kuwasilisha maamuzi yake kwa pamoja.

Kila mwaka mnamo Septemba, Rais wa Tume ya Ulaya hulihutubia bunge la Umoja wa Ulaya ambapo katika hutoba yake hutaja  mafanikio ya mwaka uliopita na kutoa vipaumbele vya mwaka ujao. Katika hotuba yake ya mwaka huu bwana Juncker pia ameelezea jinsi Tume hiyo ya Ulaya itakavyo zikabili changamoto kubwa zinazokabili Umoja huo.

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef