Kabila aashiria ushindi nchini DRC
3 Desemba 2011Kwa mujibu wa matokeo yaliotangazwa jana, karibu asilimia 15 ya kura zilizohesabiwa zinaonesha kuwa Kabila anaongoza kwa zaidi ya kura milioni 1.52 - hiyo ni takriban kura asilimia 52.
Tshisekedi ambae ni miongoni mwa wagombea 11, ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 997,074 au asilimia 34. Rais wa Tume ya Uchaguzi, Daniel Ngoy Mulunda ametoa matokeo hayo ya awali, ikiwa ni siku nne baada ya kufanyika uchaguzi, jumatatu iliyopita.
Waandalizi wa uchaguzi, wametoa mapema baadhi ya matokeo hayo ili kukabili tarakimu za bandia zinazosambazwa kwa kutumia ujumbe wa simu za mkononi na katika tovuti. Habari hizo za uongo zimesababisha mivutano.
Wadakuzi wa mtandao walisambaza matokeo ya bandia kwenye tovuti ya afisa wa Tume ya Uchaguzi, ambayo yameonyesha kuwa Tshisekedi anaongoza kwa kiasi kikubwa. Msemaji wa Tume ya Uchaguzi, Matthieu Mpita, alinukuliwa akisema kuwa wadakuzi wameingia katika tovuti yao.
Awali shirika la haki za binadamu "Human Rights Watch" lenye makao yake makuu nchini Marekani, lilisema kuwa kiasi ya watu 18 wameuawa kabla ya uchaguzi huo kuanza katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wengi wao walipigwa risasi na wanajeshi kutoka kikosi cha walinzi wa Rais Joseph Kabila.
Matokeo kamili yanategemewa kutolewa Desemba 6 na baadae lazima yathibitishwe na Mahakama Kuu.
Mwandishi: Sudi Mnette/RTRE
Mhariri: Martin,Prema