1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabila kuapishwa leo

Mohammed Abdulrahman20 Desemba 2011

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anaapishwa leo kwa muhula wa pili wa miaka mitano, baada ya kutangazwa mshindi wa urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Novemba 28, huku hali ya wasiwasi ilitanda.

Joseph Kabila
Joseph KabilaPicha: picture alliance/dpa

Kuapishwa kwake kunafuatia kuidhinishwa kwa ushindi wake na Mahakama Kuu mjini Kinshasa, hatua ambayo imesababisha kupamba moto kwa mvutano na kiongozi wa chama cha upinzani cha UDPS, Etienne Tshisekedi, ambaye ameyakataa matokeo na kujitangaza kuwa rais.

Kwa upande mwengine Tshisekedi mwenye umri wa miaka 78, amesema kwamba ataapishwa na umma Ijumaa ijayo katika uwanja wa michezo mjini Kinshasa. Sambamba na hayo alisema mawaziri wote na magavana wa majimbo wamefutwa kazi, akitaka pia rais Kabila akamatwe. Tshisekedi aliwahi pia kujitangaza Waziri mkuu mara kadhaa , enzi ya kiongozi wa zamani Mobutu Sese Seko, alipokuwa akivutana na kiongozi huyo wa zamani.

Kabila mwenye umri wa miaka 40 anapishwa leo kukiwa na hali ya wasi wasi, kutokana na msimamo wa Tshisekedi, huku kukitolewa wito kuitaka jumuiya ya kimataifa iingilie kati na kuinusuru Congo kuingia katika machafuko mengine ya kisiasa .

Etienne Tshisekedi (kushoto) na Joseph Kabila.Picha: picture alliance/dpa/DW-Fotomontage

Wiki iliyopita viongozi wa Burundi, Jamhuri ya Afrika Kati, Kenya, Uganda, Tanzania na Zambia, waliokuwa wakihudhuria mkutano kuhusu eneo la maziwa makuu mjini Kampala, walimpongeza Kabila kwa ushindi wake, licha ya uchaguzi huo kukosolewa na Umoja wa Ulaya na waangalizi kutoka kituo cha Cater, ambao walitaja juu ya wizi wa kura na matatizo mengine yaliyolitia dosari zoezi hilo.

Kabila, aliye madarakani tokea 2001, alitangazwa mshindi kwa asilimia 49 dhidi ya 32 ya kura za mpinzani wake mkuu Tshisekedi.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman
Mhariri: Mohammed Khelef

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW