1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kabila kuondoka madarakani baada ya uchaguzi

Isaac Gamba
1 Januari 2017

Wanasiasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamefikia makubaliano yanayotoa wito kwa Rais Joseph Kabila kuondoka madarakani baada ya uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Demokratische Republik Kongo Joseph Kabila in Bata
Picha: Getty Images/AFP/C. De Souza

Makubaliano hayo yaliyotiwa saini Jumamosi (31 Disemba 2016) yanalenga kumaliza mkwamo wa kisiasa uliolikumba taifa hilo na kusababisha vurugu baada ya vikosi vya usalama kupambana na makundi ya waandamanaji.

Chini ya makubaliano hayo, Rais Joseph Kabila atasalia madarakani hadi mwishoni mwa mwaka 2017, huku pakiundwa baraza la mpito litakaloongozwa na kiongozi wa upinzani, Etienne Tshisekedi, na waziri mkuu kuteuliwa kutoka upande wa upinzani wenye nguvu.

Hatua hiyo inafuatia mazungumzo yaliyoanzishwa na Kanisa Katoliki baada ya vurugu kubwa kumpinga Rais Kabila kuendelea kubakia madarakani baada ya muda wake kumalizika tarehe 20 Disemba, huku akiwa hana dalili za kutangaza kujiuzulu na pia kuitisha uchaguzi mwingine katika siku za karibuni.

Kwa mujibu wa waraka wa makubaliano hayo, ambao pia umeshuhudiwa na shirika la habari la AFP,  Rais Kabila amethibitisha kuwa hatawania tena muhula wa tatu wa uongozi, na upinzani nao umemkubalia kusalia madarakani hadi atakapokabidhi madaraka kwa rais atakayechaguliwa baadaye mwaka huu.

Kanisa Katoliki, ambalo lina mchango mkubwa katika kuleta uthabiti ndani ya taifa hilo la Afrika ya Kati lenye kiasi cha watu milioni 70, lilianzisha mazungumzo hayo Disemba 8 na awali lilikusudia makubaliano yawe yamefikiwa kabla ya sherehe za Krismasi, ingawa muda huo ulipita.

"Tumeyapokea kwa furaha hatua hii iliyofikiwa," alisema Askofu Marcel Utembi, mmoja wa viongozi wa kanisa walioandaa mazungumzo hayo.

 

Monusco yapongeza hatua hiyo

Mmoja wa wanajeshi wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa- MonuscoPicha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Kiongozi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo (MONUSCO), Maman Sidikou, pia alipongeza makubaliano hayo, lakini akasema ni lazima kazi ya ziada ifanyike "kuhakikisha kuwa kila kipengele kinatekelezwa" ili kulinda uthabiti wa kisiasa.

Wapiga kura awali walitarajia kumchagua rais mpya katika mwaka 2016, lakini serikali ikatangaza kuwa daftari la watu waliosajiliwa kupiga kura lazima lipitiwe upya katika taifa hilo ambalo ukubwa wake ni karibu sawa na bara la Ulaya. Hatua hiyo ilifuatiwa na uamuzi wa mahakama ya katiba uliozua utata mkubwa kwa kumpa Rais Kabila nafasi ya kusalia madarakani hadi uchaguzi mwingine utakapoitishwa.

Upinzani ulidai kuwa Rais Kabila anapanga kufanya marekebisho ya katiba yatakayompa nafasi ya kuwania muhula wa tatu wa uongozi.

Kabila, mwenye umri wa miaka 45, amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 kufuatia kuuawa kwa baba yake, Laurent Kabila.

Alithibitishwa kuwa kiongozi wa taifa hilo mnamo mwaka 2006, wakati ulipofanyika kwa mara ya kwanza huru tangu taifa hilo lilipopata uhuru wake kutoka Ubeligiji mwaka 1960.

Kabila alichaguliwa tena kwa muhula wa pili mwaka 2011 katika uchaguzi unaolezwa kugubikwa na udanganyifu.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW