Kabuga atafikishwa kizimbani Septemba 29
18 Agosti 2022Jaji wa mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa Iain Bonomy amesema hoja za ufunguzi zitaanza Septemba 29 na kisha ushahidi kuanza kusikilizwa Oktoba 5.
soma Mahakama Ufaransa kutoa hukumu dhidi ya Kabuga
Kabuga, mwenye umri wa miaka 87, alifikishwa mahakamani leo akiwa kwenye kiti cha magurudumu. Mwezi Juni, majaji wa mahakama ya ICC walikataa ombi la utetezi, kwa kuamuru kuwa Kabuga yuko katika hali nzuri kiafya kuweza kufunguliwa mashitaka.
Bonomy alisema mshtakiwa atafikishwa kizimbani mara tatu kwa wiki, na kila kiko cha mahakama kikidumu kwa masaa mawili. Aidha, amesema kuwa mtuhumiwa huyo ataendelea kuzuiliwa katika kizuizi cha mahakama hiyo kilicho umbali wa kilomita chache na ikilazimika ataruhusiwa kushiriki kwa njia ya video.
Kabuga akabiliwa na mashitaka sita
Mtuhumiwa huyo alikamatwa Mei 16 mwaka wa 2020 katika kitongoji cha mji mkuu wa Ufaransa Paris baada ya miaka 25 ya kuwa mafichoni.
soma Mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda akamatwa
Kabuga anakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la mauaji ya halaiki na matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, mateso, na mauaji. Akiwa kizimbani alisikiliza kwa makini na aliiambia mahakama kuwa alitaka kubadilisha mawakili.
Wakili wake wa utetezi wa sasa Emmanuel Altit, alikana mashtaka kwa niaba ya mteja wake wakati Kabuga alipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba 2020.
soma Waendeshamashtaka wa ICC wataka Kabuga apelekwe The Hague.
Waathirika wadai haki
Akijibu tangazo la kesi ya Kabuga lililotolewa Alhamis, Egide Nkuranga wa muungano wa waathirika wa mauaji ya kimbari IBUKA alisema kesi hiyo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu licha ya kile alichokitaja kama "mbinu za kuchelewasha zinazotumiwa na mawakili wa Kabuga."
Nkuranga amenukuliwa na shirika la habari la AFP akisema, "Tunataka haki ipatikane, kwa hivyo kesi yake inahitaji kuharakishwa, Kabuga akifa kabla ya kuhukumiwa, atakufa kwa kudhaniwa kuwa hana hatia, na hii itakuwa mbaya kwa haki".
Umoja wa Mataifa unasema watu 800,000 waliuawa nchini Rwanda mwaka 1994 katika mauaji ya kikatili ya siku 100 yaliyoushangaza ulimwengu. Zaidi ya mashahidi 50 wanatarajiwa kufika kwa upande wa mashtaka, ambao ulisema walihitaji takriban saa 40 kumaliza kesi yao.
//AFPE