KABUL: Mateka wa Korea Kusini waachiliwa huru
31 Agosti 2007Matangazo
Baada ya mateka 19 wa Korea Kusini kuachiliwa huru na wanamgambo wa Taliban,serikali ya Seoul imekosolewa kwa sababu ya kufanya majadiliano ya moja kwa moja pamoja na Wataliban.Waziri wa Masuala ya Nje wa Afghanistan,Rangin Dadfar Spanta amesema,utakuwa ujumbe wa hatari ikiwa kutazushwa fikra kuwa jumuiya ya kimataifa na serikali ya Afghanistan zinaweza kushinikizwa. Waziri wa Masuala ya Nje wa Kanada,Maxime Bernier pia amesema,majadiliano hayapaswi kufanywa pamoja na Taliban.
Magazeti mengi nchini Korea Kusini yanahofu kuwa sifa ya nchi hiyo katika jumuiya ya kimataifa imeathirika kwa sababu ya kujadiliana moja kwa moja na Taliban.Siku ya Alkhamisi wanamgambo wa Taliban waliwaachilia huru mateka saba wa mwisho wa Korea Kusini.