KABUL:Baraza la Jirga lapendekeza kuondolewa kwa vikosi vya NATO
10 Agosti 2007Baraza la viongozi wa kikabila kutoka Afghanistan na Pakistan JIRGA linatoa wito wa majeshi ya mataifa ya magharibi kuondolewa nchini Afghanistan na nafasi yake kuchukuliwa na majeshi ya kiislamu.
Kulingana na kiongozi mmoja wa Pakistan aliyekuwa mbunge,Malik Fazel Manaan Mohmad majeshi ya NATO na vikosi vinavyoongozwa na Marekani nchini Afghanistan ndio chanzo cha usalama duni.
Nchi ya Pakistan ilisaidia Afghanistan kufurusha majeshi ya Urusi katika vita vya Jihad lakini kwa sasa majeshi ya mataifa ya kigeni ndiyo yanayoisaidia.Wito huo unatolewa wakati kikao cha Jirga kinaingia siku yake ya pili kujadilia tatizo la Al Qaeda na Taliban.
Kikao hicho cha Jirga kilifunguliwa na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan na washirii kutoa wito wa ushirikiano zaidi ili kupambana na ghasia.Mkutano huo ni wa kwanza wa aina yake.