Mzozo wa Rwanda/Ujerumani
12 Novemba 2008Licha ya serikali ya Rwanda kuchukua hatua kali ya kumfukuza balozi wa Ujerumani, Ujerumani itampeleka Ufaransa mkuu wa itifaki wa Rwanda,Rose Kabuye aliekamatwa na polisi wa Ujerumani kwenye uwanja wa ndege wa Frankfurt jumapili iliyopita.
Msemaji wa idara ya mashtaka ya mji wa Frankfurt amethibitisha leo kuwa Rose Kabuye atapelekwa Ufaransa baada ya mahakimu wa Ujerumani kutoa hukumu hiyo.Na serikali ya Ujerumani imesema kuwa haina kipingamizi katika hilo.
Rose Kabuye ambae ni mkuu wa itifaki nchini Rwanda alikamatwa kufuatana na msingi wa waranti wa kimataifa uliotolewa na Ufaransa. Kabuye anatuhumiwa kuhusika na mauaji ya rais Juvenal Habyarimana aliekuwa mhutu. Habyarimana aliuawa kutokana na ndege aliyokuwa amepanda kutunguliwa.
Ufaransa inasema kuwa mauaji hayo ndiyo yalikuwa chanzo cha maauji halaiki yaliyotendeka nchini Rwanda mnamo mwaka 1994.
Watu hadi laki nane, watusi na wahutu waliokuwa na mtazamo wa ukadirifu waliangamizwa.
Rais Paul Kagame wa Rwanda amesema Ujerumani imehujumu uhuru wa nchi yake kwa kuchukua hatua ya kumkamata bibi Kabuye. Rais Kagame amesema hatua hiyo ni kitendo cha cha ujuvi.
Serikali ya Rwanda imelipiza kisasi kwa kumfukuza balozi wa Ujerumani nchini. Balozi huyo ameambia kuondoka nchini Rwanda mnamo muda wa saa 48.Rwanda pia imemrejesha nyumbani balozi wake kwa ajili ya mashauriano.
Lakini serikali ya Ujerumani imesema , haikuwa na njia nyingine ila kumkamata afisa Kabuye katika msingi wa waranti wa kimataifa uliotolewa na Ufaransa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Jens Plötner ameeleza kuwa polisi ya Ujerumani imemkamata Kabuye kisheria .
Lakini hatua ya kukamatwa mpambe wa rais Kagame, Rose Kabuye imesababisha hasira nchini Rwanda. Maalfu ya wanyarwanda wamefanya maandamano makubwa na kuenda kwenye ubalozi wa Ujerumani na kwenye ofisi za radio Deutschewelle mjini Kigali.
Bibi Rose Kabuye amekanusha madai ya mauaji na kuhusika na ugaidi.