1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kadhia ya Hans-Georg Maaßen Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Septemba 2018

Kisa cha aliyekuwa mwenyekiti wa idara ya upelelezi wa ndani Hans-Georg Maaßen, jinsi waengereza wanavyokabwa na kitanzi cha Brexit na jinsi rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan nchini Ujerumani magazetini.

Hans-Georg Maassen und Horst Seehofer
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Sohn

Kisa cha aliyekuwa mwenyekiti wa idara ya upelelezi wa ndani Hans-Georg Maaßen na jinsi kilivyoitikisa serikali kuu ya muungano mjini Berlin, jinsi waengereza wanavyokabwa na kitanzi cha Brexit na jinsi rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anavyoregeza kamba kabla ya ziara yake nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini.

Tunaanzia Berlin ambako hatimae kizungumkuti kilichosababishwa na maridhiano yaliyofikiwa jumanne iliyopita kati ya wakuu wa vyama vitatu vinavyounda serikali kuu ya muungano, Angela Merkel wa CDU, Horst Seehofer wa CSU na Andrea Nahles wa SPD kimemalizika bila ya serikali kuvunjika. Aliyekuwa mwenyekiti wa idara ya upelelezi wa ndani Hans Georg Maaßen amehamishiwa wizara ya ndani na hatopandishwa cheo kinyume na ilivyotangazwa hapo awali. Gazeti la Badische Zeitung linaandika: "Si kawaida kuiona serikali kuu ya muungano kubadilisha uamuzi wake baada ya kupita siku chache tu, kwasaabu ya ghadhabu miongoni mwa wananchi.

Cha kutia moyo ni jinsi  mwenyekiti wa SPD Andrea Nahles, alivyoweza, hata kama ni kutokana na shinikizo , kukiri amefanya makosa na kufanikiwa baadae kuwatanabahisha viongozi wote wawili wa vyama ndugu vya CDU/CSU, Angela Merkel na Horst Seehofer. Makubaliano hayo yanabainisha viongozi hao wapenia kuinusuru serikali kuu ya muungano. Kama dhamiri yao inatosha kukabiliana na changamoto zilizoko, hilo ni suala jengine."

Vyama vikuu vimepoteza uhusiano mashinani

Gazeti "Emder Zeitung linahisi vuta ni kuvute inadhihirisha vyama hivyo vitatu vikuu vimepoteza uhusiano mashinani. Gazeti linaandika:" Watu wanaweza kwenda umbali wa kusema hawajui matatizo ya aina gani yako nchini. Wanajifikiria wao tu. Mwenye kufuata msimamo kama huo asishangae mkondo wa kisiasa ukimgeukia. Kadhia ya Maaßen ilifurutu , sihaba imemalizika bila ya udhia."

Brexit yageuka mchezo wa "House of Cards"

 Miezi sita kabla ya Uengereza kujitoa rasmi katika Umoja wa Ulaya-Brexit, hakuna maridhiano yaliyofikiwa si kati ya Uengereza na Umoja wa Ulaya na pia si kati ya waengereza wenyewe kwa wenyewe. Gazeti la "Nordwest-Zeitung" linajiuliza : "Eti kinachoshuhudiwa katika kadhia ya Brexit ni tamthilia ya kusisimua ya kisiasa au ni yote ni kweli? Mkakati wa Theresa May miezi sita kabla ya Uengereza kujitoa katika Umoja wa ulaya unalingana na  mchezo wa"House of Cards". Mwisho haujulikani, kila kipindi kinachofuata mambo yanazidi kuwa magumu, ufumbuzi haujulikani utakuwa wa aina gani."

Erdogan kuitembelea Ujerumani

Tunamalizia yaliyoandikwa magazetini kwa ripoti kuhusu ziara ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan nchini Ujerumani. Erdogan anataka kuzungumza linaandika gazeti la "Frankenpost": "Nyumani kunatokota , uchumi unazorota. Na kwakuwa uhusiano pamoja na wakubwa wa dunia hii, marafiki zake wepya, Donald Trump na Vladimir Putin aliokuwa akiwategemea, umeingia ila, angependelea kumlaani shetani. Wajerumani wanabidi wamsaidie. Na wanastahiki pia. Lakini ikiwa nchi yake itaendelea kuwa jela kubwa, basi atakuwa anaiwekea  mwenyewe vizuwizi njia kuelekea uhusiano mwema kati ya Ujerumani na Uturuki."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW