1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame: Amani ya kikanda ni kipaumbele cha Rwanda

Hawa Bihoga
12 Agosti 2024

Rais wa Rwanda Paul Kagame amesema amani ya kikanda ni "kipaumbele chake" katika kukabiliana na mzozo unaoendelea kwenye nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Huku mzozo ukiendelea kufukuta baina ya nchi hizo.

Rwanda | Kigali | Rais Paul Kagame na Jeannette Kagame
Rais Paul Kagame wa Rwanda akihutubia baada ya kula kiapo kuongoza taifa hilo kwa muhula mwingine pembeni ni mkewe Jeannette Kagame.Picha: Presidency Of Rwanda/Anadolu/picture alliance

Kagame ameyasema hayo mbele ya viongozi kadhaa wa nchi na mataifa mengine ya Afrika ambao walihudhuria sherehe za kuapishwa kwake mjini Kigali.

Kiongozi huyo, ambaye anatajwa kuiongoza Rwanda kwa mkono wa chuma tangu kumalizika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ,aliahidi kulinda amani, mipaka ya taifa hilo na kuleta umoja wa kitaifa.

Aidha taifa hilo dogo la Afrika Mashariki, ambalo limepitia pandashuka chungumzima ikiwemo vita vya wenyewe kwa wenyewe, linashutumiwa kwa kuchochea ukosefu wa utulivu katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaopambana na jeshi la Kinshasa.

Soma pia:Kagame aapishwa aksiema amani ya kanda ni 'kipaumbele' cha Rwanda

 "Amani katika eneo letu ni kipaumbele kwa Rwanda lakini bado imekuwa ikikosekana, hasa katika eneo la mashariki mwa Kongo."

Alisema punde tu baada ya kula kiapo na kuongeza kwamba "amani haiwezi kutolewa na yeyote au pahala popote bila kujali nguvu inayotumia, ikiwa pande inayohusika haiwajibiki kuleta kile kinachohitajika." 

Matokeo ya uchaguzi wa Julai 15 ambayo yalimrejesha madarakani Rais Kagame kwa kupata ushindi wa asilimia 99.18 yanashutumiwa vikali na wanaharakati wa haki za binaadamu wakisema ni ukumbusho tosha wa utawala dhalimu nchini Rwanda.

Wagombea wawili tu ndio walioidhinishwa kugombea dhidi yake, huku wakosoaji kadhaa mashuhuri wakizuiliwa.

Juhudi za kusaka amaani mashariki mwa Kongo

Rais Joao Lourenco wa Angola  ni miongoni mwa waliohudhuria sherehe hizo za kuapisho kwa Kagame ambao wanatarajiwa kuwa na mazungumzo ya faragha kuhusu usitzishwaji wa mapigano eneo la Mashariki mwa Kongo yaliyokatishwa mwezi uliopita.

Luanda iliandaa makubaliano hayo baada ya mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa Kongo na Rwanda.

Ufafanuzi: Nani yupo nyuma ya mzozo wa Kongo?

02:01

This browser does not support the video element.

Hata hivyo, mnamo Agosti 4, siku ambayo usitishaji mapigano ulipaswa kuanza, waasi wa M23 ambao wameendesha makabiliano makali eneo la mashariki tangu kuanza mashambulizi mapya mwishoni mwa 2021  waliuteka mji wa mpakani na Uganda.

Soma pia:M23 wachukua udhibiti wa sehemu kubwa ya Rutshuru

Hivi karibuni ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa walisema kupitia ripoti yao kwamba wanajeshi wa Rwanda wapatao 3,000 hadi 4,000 wameungana na waasi wa M23 kupigana na kwamba "Kigali inaunga mkono kwa asilimia kubwa" oparesheni za kundi hilo.

Katika mahojiano juu ya suala hilo, mara zote Kagame hajawahi kanusha wazi uwepo wa majeshi ya Rwanda nchini Kongo, badala yake amezungumzia "mateso" ya Watutsi walio wachache na hatari ya kukosekana kwa utulivu kwenye mpaka wa Rwanda.

Hata hivyo, ndani ya Rwanda rais Kagame anasikifika kwa kulijenga taifa lake mara baada ya mauaji ya Kimbari, wakati Wahutu wenye itikadi kali walipowashambulia Watutsi walio wachache, na kuua takriban watu 800,000, hasa Watutsi na baadhi ya Wahutu wenye msimamo wa wastani.