1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame amtuhumu Tshisekedi kutumia M23 kuahirisha uchaguzi

1 Desemba 2022

Rais wa Rwanda Paul Kagame amemshtumu mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi kutumia mzozo wa kivita unaoendelea eneo la mashariki mwa nchi yake kuchelewesha uchaguzi.

Felix Tshisekedi und Paul Kagame | Präsidenten DR Kongo und Ruanda
Picha: SIMON WOHLFAHRT/AFP/Getty Images

Mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Congo na waasi wa kundi la M23 mashariki mwa Congo yamechochea zaidi mzozo na Rwanda, ambayo Congo inaishtumu kuunga mkono uasi wa kundi hilo, madai ambayo Rwanda inayakanusha.

Mazungumzo kati ya Congo na Rwanda nchini Angola wiki iliyopita yalizaa mapatano ya kusitisha mapigano, na siku kadhaa baadae, mapatano hayo yanaonekena kuendelea kuheshimiwa.

Soma pia:Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya uchaguzi mkuu Desemba 2023. 

Katika hotuba ya kiserikali, Kagame alisema "dunia nzima" inaelekeza lawama za mzozo huo kwa Rwanda lakini ni rais wa DRC Felix Tshisekedi anaetafuta kujinufaisha kutokana na machafuko hayo mnamo wakati uchaguzi ukikaribia.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (katikati) alikutana na Kagame na Tshikesedi mjini New York Septemba 21, 2022 katika juhudi za kufanya usuluhishi.Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

"Tatizo hili linaweza kutatuliwa ikiwa nchi moja inayoelekea kenye uchaguzi mwakani, haijaribu kuunda mazingira ya dharura ili uchaguzi usifanyike", Kagame alisema katika hafla ya kuwaapisha mawaziri wapya.

Soma pia: Waasi wa M23 wajitenga na mapatano ya kusitisha mapigano

"Ikiwa anajaribu kutafuta njia nyingine ya kuahirisha uchaguzi ujao, basi ingekuwa vyema akatumia visingizio vingine,na siyo sisi."

CENI: Hali ya usalama kutoa changamoto kwa uchaguzi

Tshisekedi aliingia madarakani Januari 2019 na DRC itafanya uchaguzi wa rais Desemba 2023.

Soma pia: Kenyatta na Kagame waitaka M23 kusitisha mapigano na kujiondoa mashariki mwa Kongo

Tume ya uchaguzi ya nchi hiyo CENI, ilisema mwezi uliopita kwamba ukosefu wa usalama unaoendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi yatasabisha changamoto kwa kura huru, ya kidemokrasia na ya wazi.

DRC na Rwanda zimeshtumiana kwa kuunga mkono makundi ya waasi na kurejea tena kwa M23 kumezidisha upya mzozo wa kidiplomasia baina ya mataifa hayo.

Vita vya M23 vinaathiri pia wakazi wa Bukavu

02:40

This browser does not support the video element.

Chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano yalioanza kutekelezwa Novemba 25, wapiganaji wa M23 walipaswa kujiondoa kutoka maeneo walioyakalia mashariki mwa Congo, na kushindwa kufanya hivyo kikosi cha Afrika Mashariki kitaingilia kati kuwalaazimisha.

Duru nyingine ya mazungumzo na makundi ya waasi iliendelea nchini Kenya siku ya Jumatano, bila kuwepo wawakilishi wa M23.

Mpatanishi wa mazungumzo hayo, rais wa zamani wa Kenya, Uhuru Kenyatta, alisema makundi ya waasi ya kigeni yanayoendesha shaghuli zao nchini Congo yanapaswa kuondoka au yakabiliwe na majeshi ya DRC na Afrika Mashariki.

Tayari wamepewa ilani: DRC haitakuwa mahala pa mapigano ya mataifa mengine, alisema Kenyatta.

Chanzo: AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW