1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Kagame ataja "undumila kuwili" kuhusu mzozo wa DRC

17 Januari 2025

Rais Paul Kagame wa Rwanda kwa mara nyingine tena ameilaani jamii ya kimataifa ambayo imekuwa ikikosoa demokrasia nchini Rwanda.

Paul Kagame | Rwanda
Rais Paul Kagame wa RwandaPicha: Lim Yaohui/Newscom/Singapore Press Holdings/IMAGO

Ni hotuba iliyodumu kwa muda wa saa moja na sekunde hamsini ambapo Rais Kagame amegusia mambo mengi kuhusu siasa za maziwa makuu ikiwa ni pamoja na usalama, demokrasia na shutuma za hapa na pale kuhusu Rwanda

Vita vya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongovimechukua nafasi kubwa katika hotuba yake ambapo jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu Kongo limeitaja Rwanda kulisaidia kwa hali na mali kundi la M23 linaloendelea kuyachukua maeneo mengi katika eneo hilo la mashariki mwa Kongo.

Juhudi za kutatua mzozo zimefikia wapi?: Mazungumzo ya amani kati ya Kongo na Rwanda yashindikana, na kutishia mchakato wa amani

Lakini rais Kagame kwa mara nyingine akifafanua amesema; "Tunaishi katika ulimwengu ambapo sasa ushahidi wa kimantiki, vidhibitisho na ukweli wa mambo havipewi umuhimu tena, kinachopewa uzito ni kile ambacho amekisema mtu mwingine hata kama hakina ukweli, tumebebeshwa mzigo mzito katika mzozo huu bila kujali uongo wa lawama zinazotolewa dhidi yetu."

Amesema Rwanda inalaumiwa tu kwa sababu jamii za mashariki mwa Kongo zinazotumia lugha ya Kinyarwanda zina mafungamano na Rwanda tangu enzi za ukoloni ilipochorwa mipaka ya mataifa.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix TshisekediPicha: DW

Ameilaani jamii ya kimataifa ambayo kwa miaka 30 iliyopita imeshindwa kuutatua mzozo huu huku kifahamu fika mzizi wa tatizo.

"Ni mrejesho gani katika uwekezaji mkubwa kikosi kikubwa kama kile cha umoja wa mataifa nchini Kongo?Cha shirika kubwa kama umoja wa mataifa,kikosi chenye kutumia kiasi kikubwa cha pesa, unapata faida gani zaidi ya hali kuendelea kuharibika zaidi, hivi ukiwauliza kwa takribani miongo mitatu MONUSCOimefanya kazi gani watajibu nini? Hakuna kitu, na hii inakunyesha kuwa ndiyo sababu siku wanaulaumu Rwanda kama njia ya kukwepa majukumu yao."

Soma: Waziri wa Kongo ataka kumkamata Kagame, akimwita "mhalifu"

Rais Kagame amesema kwamba lawama za jamii ya kimataifa kwa serikali yake haziwezi kusaidia lolote, akaonya kwamba bila kutatua chanzo  cha mzozo huu utaendelea kukua.

"Kama unadhani Rwanda iko mashariki mwa DRC kusababisha matatizo unatakiwa kujiuliza kwa nini imeamua kwenda pale kupigana, pengine hiyo itakusaidia kuelewa baadhi ya vitu ulitakiwa kufanya kutuliza hali ya mambo, lakini kuendelea kutoa ripoti na kutishiatishia haisaidii lolote ngoja niwaeleze tumeteseka vya kutosha katika miaka 30 iliyopita hatuwezi kamwe kukubali kurudi kule tulipotoka haijalishi uwezo na ukubwa wa watesi wetu."

Tshisekedi: Amani imo mikononi mwa rais atakayemrithi Kagame

07:56

This browser does not support the video element.

Mzozo wa mashariki mwa Kongo umesababisha uhusiano wa Rwanda na Kongo kuharibika katika kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi ametishia mara kadhaa kupitia hotuba zake kuwa ataishambulia Rwanda na kuondoa utawala mjini Kigali.Lakini Kagame akionekana kumjibu kwa mara nyingine tena amesema

"Mtu anayesababisha matatizo katika mzozo huu tunaozungumzia huyu bwana Tshisekedi hajachaaguliwa,  hata mara moja mihula miwili ya utawala wake hajachaguliwa, na hilo mnalitambua na ndiyo maana awali nimesema siku hizi hakuna kujali ukweli wa kimantiki, vidhibitisho kinachotazamwa ni maslahi, hajachagukiwa ninyi mnajua pia, tofauti hamsemi wazi lakini mimi nayasema wazi," alisema Rais Kagame.

Soma pia: Kagame: Amani ya kikanda ni kipaumbele cha Rwanda

Ripoti ya jopo la watafiti wa Umoja wa Mataifa iliyotolewa siku ya Alhamis imeitaja serikali ya Kinshasa kuwasaidia wanamgambo wa kihutu wa FDLR ambao wameshatangaza harakati za kutangaza vita dhidi ya Rwanda. Hali hii pamoja na serikali ya Kinshasa kukataa kufanya mazungumzo na kundi la M23 linaliweka tumaini la kumalizika kwa vita katika hali isiyotabirika.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW