1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame ataka Afrika kushirikiana zaidi kwenye ulinzi wa anga

Admin.WagnerD25 Januari 2022

Rais Paul Kagame wa Rwanda amezitaka nchi za kiafrika kuwa na ushirikiano zaidi katika ulinzi wa anga wakati hali ya usalama inapozidi kudorora katika baadhi ya mataifa ya kiafrika.

Ruanda Paul Kagame  Goma Kongo
Picha: Giscard Kusema

Rais Kagame ambaye nchi yake ina majeshi ya kulinda amani kwenye nchi kadhaa za kiafrika ameyasema hayo mjini Kigali alipokuwa akifungua kikao cha siku nne cha wakuu wa majeshi ya anga kutoka nchi 30 za Afrika. 

Kikao hiki kinachofanyika kwa ushirikiano na kikosi cha anga cha Marekani katika nchi za kiafrika na Ulaya na lengo ni kutathmini ushirikiano unaoendelea baina ya jeshi la anga la Marekani katika nchi za Afrika na Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na visa vinavyohatarisha usalama katika kanda ya nchi hizo.

Soma Zaidi: Vikosi vya Msumbuji, Rwanda vyakomboa mji muhimu

Wakuu wa majeshi ya anga kutoka nchi hizo 30 kila mmoja atapata nafasi ya kufafanua changamoto zinazolikabili jeshi lake na mikakati inayochukuliwa kuhakikisha usalama wa kimkakati unafikiwa. Katika ufunguzi wa kikao hiki ambacho kinafanyika wakati dunia ikikabiliwa na virus hatari vya corona imesemekana kwamba hakuna nchi hata moja ambayo bila ushirikiano na nchi nyingine inaweza kutimiza ndoto ya usalama endelevu.

''Usafiri wa kimkakati wa anga hii leo unapaswa kupewa kipaumbele kuliko hata majanga mengine. Na katika kikao hiki cha wakuu wa majeshi ya anga...hili linapaswa kutazamwa kwa upana wake ili tujue ni kwa kiasi gani moja ilnaweza kuisadia nyingine linapokuja suala la usafirishaji wa zana za usalama. Na hata ukitazama vizuri utaona kwamba hata suala hili la corona limetuonyesha kwamba tunahitaji kushirikiana. Kwa hiyo ni jukumu letu kuendelea kushirikiana kwa ajili ya kutambua zaidi changamoto za usalama katika bara zima.'' alisema Peter Vrooman, balozi wa Marekani anayeondoka Rwanda.

Rais Paul Kagame wa Rwanda na Filipe Nyusi wa Msumbiji walipoyakagua majeshi kutoka Rwanda yaliyotumwa Msumbiji kurejesha usalama katika jimbo la Cabo DelgadoPicha: Simon Wohlfahrt/AFP/Getty Images

Rwanda kama nchi iliyoandaa na kupokea kikao hiki cha wakuu wa majeshi ya anga imesema kwamba bara la Afrika na uliwengu kwa ujumla linakabiliwa na changamoto za kiusalama lakini mara nyingi unakuta tatizo lililopo ni ushirikiano usiotosha hali ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikitoa mianya kwa wahalifu hasa wale wanaofanya ughaidi wa kuvuka mipaka.

Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye amekifungua rasmi kikao hiki amesema kwamba usalama na amani ni msingi wa maendeleo endelevu kwa kila nchi hivyo kuimarisha usalama huo si jambo ambalo linawezekana bila ushirikiano wa mataifa

Alisema ''Uwezo wa harakati zetu za anga una changamoto, sekta ya operesheni za majeshi ya anga barani Afrika haina uwezo wa kujibu tena kwa haraka changamoto za usalama mdogo kwenye anga zetu. Kiasi kikubwa cha changamoto za usalama wa Afrika ni zile zinazovuka mipaka na kwa mantiki hiyo hakuna nchi hata moja kwayo yenyewe ina raslimali za kutosha kukabiliana nazo peke yake. Kwa hiyo basi tunatakiwa kuweka kipaumbele katika ushirikiano wetu. Faida za kufanya kazi pamoja ziko wazi.''

Imesemekana kwamba ni ushirikiano huo unazisaidia nchi kama Rwanda kupeleka silaha za kijeshi kwa wanajeshi wa nchi wanakolinda usalama. Ushirikiano wa majeshi ya anga ya Marekani barani Afrika na katika nchi za bara ulaya umetajwa kama uliosaidia katika harakati mbalimbali kuzima mashambuliziya maghaidi waliopanga njama za kushambulia baadhi ya nchi au kuingilia mfumo wake wa usalama wa anga. Ni kikao ambacho kitakamilika siku ya Ijumaa wiki hii baada ya kuchukua mikakati kadhaa.

Sylvanus Karemera.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW