1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagame: Kiongozi wa muda mrefu anayezidi kuchanja mbuga

16 Julai 2024

Paul Kagame amekuwa kiongozi wa Rwanda kwa miongo mitatu. Anasifiwa kwa kuivusha nchi baada ya mauaji ya kimbari ya 1994, lakini wakosoaji wake wanasema amebinya sauti za wapinzani na kuhatarisha demokrasia.

Paul Kagame | Rwanda
Rais Paul Kagame akipiga kura katika uchaguzi wa 2024Picha: Brian Inganga/AP/picture alliance

Wanyarwanda wengi hawamfahamu kiongozi mwingine yeyote isipokuwa Paul Kagametangu yalipomalizika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambapo zaidi ya Watutsi milioni moja na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa.

Hapo awali Kagame aliongoza kundi la wanamgambo wa Kitutsi lililokuwa na makao yake makuu nchini Uganda la Rwandan Patriotic Front (RPF), ambalo lilimaliza mauaji ya Wahutu dhidi ya Watutsi kwa kuwashinda waliohusika na kampeni ya mauaji. Mnamo mwaka 1994, baada ya mauaji ya kimbari na vita vya wenyewe kwa wenyewe, Pasteur Bizimungu ndiye alikuwa Rais wa Rwanda. Kagame wakati huo alitwaa vyeo vya umakamu wa rais na waziri wa ulinzi.

Alichukua rasmi wadhifa wa urais mwaka 2000 na tangu wakati huo hajang'oka madarakani. Ameongeza mamlaka yake nchini Rwanda kwa miaka mingine mitano, katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumatatu ya Julai 15. Ushindi wake wa zaidi ya asilimia 99.1 haujawashangaza wachambuzi wengi kwani hapakuwa na upinzani wowote wa maana.

Bango la Kagame wakati w akampeniPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Wanyarwanda wanataka Kagame abakie?

Katika kipindi cha nyuma, kiongozi huyo aliashiria kuwa atajiuzulu lakini muda mchache kabla tu ya uchaguzi wa rais wa mwaka huu, Kagame alitetea uamuzi wake wa kusalia madarakani mfululizo, akiwaambia waandishi wa habari kwamba watu wanamtaka aendelee. Alisema kuwa "kibinafsi, ninaweza kwenda nyumbani na kupumzika kwa raha, lakini chama tawala na Wanyarwanda wamekuwa wakiniomba kusimama kwa muhula mwingine."Rais Kagame ashinda uchaguzi wa Rwanda kwa kishindo

Mkazi mmoja wa Kigali Rachid Bugirimfura, aliiambia DW kwamba Rais Kagame amekuwa ni kiongozi mzuri kwa nchi hasa baada ya mauaji ya kimbari. "Kagame alihimiza umoja wa Wanyarwanda wote kwa sababu watu wengi walikuwa wameitenga nchi baada ya mauaji ya kimbari."

Hakuna Rwanda ya sasa bila Kagame

Kwa baadhi ya Wanyarwanda, bila Kagame kusingekuwa na Rwanda ya sasa, ambayo inatambulika vyema duniani.

"Aliifanya Rwanda itambulike kwenye ramani ya kimataifa jambo ambalo halikuwepo hapo awali. Kimataifa Rwanda ilijulikana kwa maisha yake mabaya ya zamani lakini sasa imebadilika." Hayo yalisemwa na Marie Louise Uwizeyimana, mkazi wa Kigali wakati alipozungumza na DW.

Umati wa wafuasi wa Kagame wakati wa kampeniPicha: Jean Bizimana/REUTERS

Kulingana na benki ya Dunia, uchumi wa Rwanda umesalia kuwa thabiti na wenye kubadilika licha ya changamoto za nje na ndani. Rwanda imefikia kiwango cha ukuaji wa asilimia 7.6 katika robo tatu ya kwanza ya mwaka 2023 huku ukuaji wa Pato la Taifa ukitarajiwa kuongezeka kati ya mwaka 2024 hadi 2026.Kura zaanza kuhesabiwa Rwanda baada ya uchaguzi mkuu

Msemaji wa serikali Yolande Makolo alipozungumza na DW alisema Rwanda chini ya Kagame iko vizuri leo kuliko ilivyokuwa nyuma. "Tumefanikiwa zaidi katika mambo muhimu zaidi tunayotaka kuyafanya, ambayo yanamaanisha ulinzi na usalama wa Wanyarwanda, kuwarejesha nyumbani wakimbizi, kuwaunganisha Wanyarwanda, haki na maendeleo kwa Wanyarwanda."

Je maendeleo yanadumaa chini ya Kagame?

Ama kwa upande mwingine, si kila mtu anavutiwa na Kagame na aina yake ya uongozi. Kiongozi wa upinzani wa Rwanda Victoire Ingabirealiiambia DW kuwa "Ni kweli kumekuwa na baadhi ya mafanikio. Ninakubali, kwamba mjini Kigali tuna majengo mazuri, zahanati na mitaa, lakini maendeleo si hayo. Maendeleo ni kuelimisha vijana."

"Nje ya Kigali, hatuna barabara, tunahitaji barabara, tunahitaji umeme, tunahitaji maji, tunahitaji hospitali, kuna mambo mengi sana ambayo lazima tuyafikie."Mahakama kuu Rwanda yamzuia Ingabire kugombea uchaguzi wa rais

Kuzuia upinzani

Shutuma nyingine zinazomkabili Kagame ni kudhoofisha sauti zinazopingana naye na hivyo kufanya iwe vigumu kwa yeyote kumpinga yeye na mamlaka yake.

Uchaguzi wa rais Rwanda: Kuna cha tofauti mara hii?

01:57

This browser does not support the video element.

Ripoti iliyotolewa na shirika la utetezi wa haki za binadamu la Human Rights Watch mwaka 2023 kuhusu Rwanda ilisema "Vyama vya upinzani vinakabiliwa na vikwazo vya kiutawala vya kujiandikisha na shinikizo la kisiasa kutaka kushikilia msimamo wa serikali. Zaidi ya wanachama 12 wa upinzani wako gerezani.”

Lakini maafisa wa serikali ya Kagame wanasema hakuna ubaya katika utawala na uongozi wake. "Hatuui watu, sisi ni nchi ya utawala wa sheria, sisi ni nchi inayothamini maisha, hilo ndilo somo kubwa ambalo tumejifunza kutokana na mauaji ya kimbari, kazi yetu ni kuwatunza Wanyarwanda, watu wana uhuru wa kusema chochote wanachokitaka,” hayo ni maneno ya msemaji wa Serikali Yolande Makolo. Rwanda: Kagame kurejea madarakani kwa muhula wa nne?

Chini ya Kagame, Rwanda imeshuhudia uhusiano na majirani zake ukizorota, haswa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambayo inamtuhumu Kagame na utawala wake kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na serikali ya Kongo. Kagame amekuwa akikana kuhusika.