1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Kagame kujadili hatma ya shujaa wa "Hotel Rwanda"

13 Machi 2023

Rais Kagame amesema kulikuwa na majadiliano juu ya “kusuluhisha” hatma ya Paul Rusesabagina, ambaye alionyeshwa kama shujaa katika filamu ya Hollywood na ambaye anatumikia kifungo cha miaka 25 jela kwa tuhuma za ugaidi.

Ruanda | Paul Rusesabagina | Prozess in Kigali
Picha: Clement Uwiringiyimana/REUTERS

Paul Rusesabagina alihukumiwa mnamo Septemba 2021 kutokana na uhusiano wake na kundi linalopinga utawala wa Kagame.

Hata hivyo alikanusha mashtaka yaliyokuwa yakimkabili na kukakataa kushiriki katika kesi ambayo, yeye pamoja na wafuasi wake walidai inaendeshwa kisiasa.

Soma pia:Wiki ya kumbukumbu ya mauwaji ya kimbari nchini Rwanda 

Marekani imesema Rusesabagina "alizuiliwa kimakosa,” kwa kiasi fulani ikitoa sababu ya ukosefu wa uwanja sawa wa kuendesha kesi hiyo.

Rusesabagina ana hati rasmi inayompa haki ya kuishi nchini Marekani.

Rais Paul Kagame amesema Rwanda haitoshinikizwa wala kutishwa juu ya hatma ya Rusesabagina, japo leo Jumatatu kiongozi huyo ameonekana kulegeza msimamo wake wa awali. Kigali imekwenda mbali zaidi na kutoa nafasi ya maelewano.

Rwanda yasema kesi ya Rusesabagina ilifuata mkondo wa sheria 

Paul Rusesabagina akizungumza na wakili wake Gatera Gashabana katika mahakama mjini KigaliPicha: Clement Uwiringiyimana/REUTERS

Katika mahojiano kwa njia ya video katika Jukwaa la Kimataifa kuhusu Usalama, Kagame alisema, "Hatukwami na wakati uliopita. Tunaangalia mbele. Kwa hivyo kuna majadiliano, tunaangalia njia zote za kutatua suala hilo bila ya kuathiri mambo ya msingi wa kesi yenyewe." 

Mnamo mwezi Agosti, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken alielezea wasiwasi wake kwa Kagame kuhusu kesi ya Rusesabagina. Hata hivyo, Rwanda imesisitiza kuwa kesi hiyo imefanyika kwa kufuata mkondo wa sheria.

Rusesabagina alicheza kama shujaa katika filamu ya Hollywood "Hotel Rwanda” kuhusiana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Filamu hiyo ilimuonyesha kama shujaa aliyehatarisha maisha yake ili kuwaokoa na kuwapa hifadhi mamia ya watu, alipokuwa meneja katika hoteli ya kifahari wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Soma pia:Mahakama ya Rwanda yamkuta Rusesabagina na hatia ya ugaidi 

Rusesabagina ambaye ni mkosoaji mkubwa wa Kagame, alikiri kushikilia moja ya nafasi za uongozi katika kundi linalompinga Kagame la Rwanda Movement for Democratic Change japo amekanusha kuhusika na mashambulizi yaliyofanywa na mrengo wa kijeshi wa kundi hilo.

Hata hivyo, majaji waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo, walisema makundi yote hayo yalikuwa na mzizi mmoja, kwa hivyo hayangetenganishwa.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema kufungwa kwa Rusesabagina, ni moja tu ya mfano wa Kagame kutumia mbinu za kiimla ili kukandamiza wapinzani wake wa kisiasa na kuongeza muda wa kuendelea kukaa madarakani. Kagame, amekanusha madai hayo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW