Kagame: Urusi ina haki ya kuwa popote barani Afrika
20 Aprili 2023Akiwa ziarani katika mataifa ya Afrika Magahribi, Rais Kagame amezungumzia wazi vita vinavyoendelea nchini Ukraine kwa kusema kwamba nchi za Magharibi zinajaribu kuiburuza Afrika katika matatizo yake, kwani baadhi ya nchi za Kiafrika zimechagua kutoegemea upande wowote katika suala hilo.
''Urusi au nchi nyingine yoyote yenye nguvu haipaswi kuwa tatizo letu. Suala ni kwamba haya mataifa makubwa yana mambo yao ya kuyatatua, halafu yanaendelea kutunyonya katika nchi zetu hizi ndogo,'' alifafanua Kagame.
Nchi kadhaa, kama vile Afrika Kusini, yenye uchumi mkubwa barani Afrika, imeenda mbali zaidi hata kuimarisha uhusiano wa kijeshi na Urusi, licha ya vita hivyo.
Afrika ina matatizo yake yenyewe
Akiwa nchini Benin, Guinea-Bissau na Guinea-Conakry, Kagame amesema nchi za Magharibi zimekuwa zikilalamika kuhusu uwepo wa China na Urusi barani Afrika, na bara hilo linapaswa kutambua mahitaji yake katika suala la ushirikiano wa kimataifa na kuwageukia wale wanaotoa kile wanachokihitaji.
Kwa mujibu wa rais huyo wa Rwanda, Afrika inajaribu kutatua matatizo yake yenyewe ambayo yanaigusa moja kwa moja, yasiyo na uhusiano wowote na nchi moja kubwa.
Aidha, amesisitiza kuwa mikataba ya ushirikiano na Urusi haihitaji kutafakari mitazamo kuhusu vita vya Ukraine. Katika ziara hiyo, Kagame ameshiriki katika shughuli kadhaa, ikiwemo kushuhudia utiaji saini wa mikataba tisa kati ya Rwanda, Benin na Guinea, pamoja na kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi wenzake.
Akizungumza katika mkutano na waandishi habari pamoja na kiongozi wa kijeshi wa Guinea, Kanali Mamadi Doumbaya, Rais Kagame amesisitiza umuhimu mkubwa wa ushirikiano wa kimataifa, iwe barani Afrika au ulimwenguni kote. Kagame ameongeza kusema kuwa kila nchi barani Afrika ina changamoto zake, lakini kushirikiana pamoja hakuna changamoto ambayo watashindwa kukabiliana nayo.
Mwanzo wa ushirikiano
Mbali na kuimarisha ushirikiano wa nchi mbili katika biashara, utawala na maeneo mengine ya kimkakati, Kagame anazidi kuonekana kama vile anashinikiza pia ushirikiano wa kijeshi na mataifa ya Afrika Magharibi katika juhudi za kuimarisha uwepo wa kijeshi wa Rwanda katika ukanda huo.
Akizungumza na DW, Waziri wa teknolojia na Mawasiliano wa Guinea, Ousmane Gaoul Diallo ameielezea ziara ya Kagame kama mwanzo wa aina mpya ya ushirikiano wa nchi za Kusini na Kusini, ambao anaamini utazinufaisha nchi zote.
Paul Melly kutoka taasisi ya wachambuzi ya Chatham House iliyoko mjini London, ameiambia DW kuwa Rwanda ina matumaini ya kuzisaidia nchi kama vile Benin, Guinea na nyinginezo, ambazo zimekumbwa na mashambulizi ya wapiganaji wa jihadi katika kipindi cha nyuma, lakini kwa ujumla zinachukuliwa kuwa haziko hatarini kama ambavyo eneo la Sahel lilivyo.
(DW)